Wakazi wa Manispaa ya Morogoro na maeneo jirani wametakiwa kujitokeza na kuona Michezo ya Majeshi Tanzania inayoanza kutimua vumbi Septemba 6 hadi 15, 2024, katika viwanja mbalinbali vilivyoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Wito huo umetolewa leo Septemba 5, 2024 na Mwenyekiti wa BAMMATA Brigedia Jeneral Saidi Hamisi Saidi wakati akiongea na waandishi wa habari kutoa taarifa rasmi ya mashindano hayo kufanyika Mkoani Morogoro.
Aidha, Brigedia Jenerali Saidi Hamisi Saidi amebainisha kuwa mgeni rasmi atakayezindua mashindano ya michezo hiyo ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambaye tayari amekwisha wasili Mkoani Morogoro.
Akifafanua zaidi, Brigedia Janeral Saidi amesema mashindano hayo yanashirikisha na kuyakutanisha majeshi ya kanda saba ambazo ni Ngome, (JWTZ) Magereza, Uhamiaji, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Zimamoto na Uokoaji, Polisi, pamoja na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akitoa wito kwa wananchi Kiongozi huyo amesema mashindano hayo hayatahusisha kiingilio chochote katika viwanja vya michezo vilivyoandaliwa ambapo ni viwanja vya Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), viwanja Umwema JKT, na viwanja vya Jamhuri, hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuangalia na kufurahia burudani za michezo ya majeahi yao ambayo ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa pete, mchezo wa masumbwi, mpira wa wavu, mpira wa mikono, kurusha mkuki, kulenga shabaha, riadha na mchezo wa vishale.
"... Nichukue fursa hii niwakaribishe wananchi katika viwanja vyote tulivyo vitangaza isipokuwa kiwanja maalum kwa mchezo wa shabaha, viwanja vingine wananchi wanakaribishwa kwa wingi kabisa ili kuja kuona burudani mbalimbali.." amesisitiza Brigedia Jeneral Saidi.
Akieleza matarajio yake, Brigedia Jeneral Saidi amesema, baada ya kumalizika mashindano hayo anaamini watakuwa na timu bora itakayoweza kushiriki mashindano mbalimbali, lakini pia watakuwa wameboresha Afya za washiriki, kuimarisha umoja na mshikamano baina ya majeshi katika utendaji kazi wao.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.