Serikali imewataka wananchi kuwa na mpango endelevu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kushirikiana na wataalam na watafiti wa mazingira ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi wenye tija.
Ushauri huo umetolewa Agosti 2, mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi wa maonesho ya nanenane kanda ya mashariki yanayofanyika katika viwanja vya nanenane vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro.
Akifafanua zaidi Mhe. Batilda amesema wananchi wanapaswa kutumia nishati safi kama umeme, gesi na mkaa mweupe ili kuepukana na mabadiliko hayo katika kutunza vyanzo vya maji, misitu na ardhi ili kutunza rutuba yake kwa uzalishaji wa mazao bora.
“… tunapaswa kuzingatia matumizi ya nishati safi kukabiliana na mabadilio ya tabia nchi…” amesema Mhe. Batilda Burian
Aidha, Balozi Batilda amesema maonesho hayo yameendelea kuwavutia wadau mbalimbali kila mwaka kwani mwaka 2023 kulikuwa na washiriki 75,000 na mwaka 2024 waliojiandikisha ni zaidi ya 80,000 na kubainisha kuwa maonesho hayo yataendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kufanya shughuli za kilimo, Uvuvi na ufugaji kwa kutumia teknolojia zaidi.
Sambamba na hilo, Mhe. Burian amesema sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi inatoa nafasi za ajira kwani 65% wanajishughulisha na kazi hizo, ambapo 28% huchangia pato la taifa, 24% ya mauzo ya bidhaa za mazao hayo nje ya nchi.
Hata hivyo Mhe. Batilda amesema serikali itaendelea kuimarisha ushirika, vikundi na majukwaa ya wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi ili kuunganisha nguvu kuwa na sauti ya pamoja katika kuimarisha matumizi sahihi ya rasilimali.
Mhe. Batilda amewasisitiza wakulima, wafugaji na wavuvi kushiriki kikamilifu na kujitokeza katika kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi na kuwachagua viongozi bora ambao watahimiza shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji na kuwasaidia katika masuala ya biashara na kuwa na tija katika taifa.
Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Kampuni ya Viridium ya Tanzania amesema kampuni hiyo imechukua hatua za mapema kuanza kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati mbadala ikiwemo mkaa mweupe ambao hutengenezwa kwa majani maalum aina ya briquettes kuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maonesho hayo hufanyika kila mwaka Agosti 8 kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ambapo kitaifa maonesho hayo yanafanyika Mkoani Dodoma.
Mwisho.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.