Mashindano ya michezo ya majeshi hapa nchini yameendelelea kupamba moto Mkoani Morogoro ikiwa leo ni siku ya tatu tangu mashindano hayo yazinduliwe rasmi Septemba 6, 2024 huku leo mchezo wa mpira wa kikapu kwa wanaume umeendelea kutisha na kuonekana ni wa kiushindani kwa timu tatu.
Mashindano hayo yamefanyika leo Septemba 8, mwaka huu katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo kwa kuzikutanisha timu sita zikiwemo SMZ, Magereza na JKT.
Mashindano ya leo kwa jumla yamejumuisha timu 6 za Uhamiaji, Polisi, SMZ, Magereza, Ngome na JKT ambapo timu tatu zimetoka na ushindi ambazo ni Polisi - 63 dhidi ya uhamiaji – 52, Magereza - 78 dhidi ya SMZ - 44 na JKT - 58 dhidi ya Ngome – 57 na kuondoka na alama tatu muhimu.
Mwalimu wa mpira wa kikapu kanda wa magereza Bw. Joseph Matley amesema malengo makubwa ya timu yao ni kupata matokeo hususan wachezaji kucheza kwa kufuata maelekezo na kujituma wakiwa uwanjani hivyo imefanya mchezo kuonekana mzuri na wa kufurahisha.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Timu ya mpira wa kikapu wa SMZ Bw. Seif Issa Omary amesema kuwa hawajafanya vizuri kwa sababu ya kuzidiwa kimbinu na kupoteza mchezo huo huku akisema tayari wachezaji wamejipanga kufanya vizuri mchezo ujao.
Naye, Nahodha wa Timu ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Bw. Felix Deogratius amesema mchezo huo ulikuwa mgumu kwa pande zote mbili kutokana na kuwa na waalimu wazoefu wa pande zote pamoja na uwezo wa wachezaji mahiri lakini mchezo umeamua kwa timu hizo tatu kuondoka na ushindi.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.