Dkt. Samia Atoa Wito kutunza miundombinu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro kutunza miundombinu ya Daraja la Berega kwa sababu daraja hilo limetumia gharama kubwa katika ujenzi wake hadi kukamilika na kwa kufanya hivyo kutapelekea lidumu na kutumika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Dkt. Samia ametoa wito huo Agosti 2, 2024 wakati akizindua Daraja la Berega linalounganisha wilaya za Gairo, Kilosa mkoani Morogoro na Kilindi mkoani Tanga ambapo hadi kukamilika kwake limetumia zaidi ya shilingi Bilioni 7
Rais Samia amesema uzinduzi wa daraja hilo umeondoa changamoto walizokuwa wakikumbana nazo wananchi wa maeneo hayo ambapo hapo mwazo walikuwa wanakwama kupita kwa sababu ya wingi wa maji, kushindwa kusafirisha mazao pia baadhi ya akina mama wajawazito wakishindwa kupita kwenda kupata huduma za kiafya katika hospitali ya Berega hivyo kusababisha hata vifo.
"... Ndugu zangu kujengewa daraja ni jambo moja, kutunzz daraja ni jambo lingine, kama mnavyojua daraja hili limetumia gharama nyingi sana naombeni tunzeni daraja.." amesisitiza Dkt. Samia
Aidha Dkt. Samia ametoa wito kwa wananchi kutunza mazingira kando ya daraja ikiwemo kutokata miti ambayo husaidia kutotanuka mto na kuathiri daraja hilo na kutochimba mchanga katikati ya daraja.
Katika Hatua nyingine Dkt. Samia amezindua hospitali ya Wilaya ya Gairo ambayo imegharimu shilingi Bilioni 4.8 ambapo imeenda kuondoa changamoto kwa Wananchi wa wilaya ya Gairo na baadhi ya vijiji vya wilaya Kongwa Mkoani Dodoma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kuzinduliwa kwa daraja hilo ni ishara ya upendo wa Mhe. Rais kwa watanzania bila ubaguzi, pia daraja hilo limepunguza adha kwa wanafunzi kutofika shuleni kutokana na maji kujaa na linaenda kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Tanga kwa sababu ya urahisi wa kusafirisha mazao.
Nae mwananchi wa kijiji cha Berega Bi. Violet Mwegoha amesema adha walizokuwa wakizipata kabla ya ujenzi wa Daraja hilo zikiwemo wagonjwa kushindwa kufika hospitali kwa wakati ambapo hupelekea vifo, pia kushindwa kusafirisha mazao kutokana na ujenzi huo adha hizo zimeondoka.
Ziara ya Mhe. Rais itaendelea Agosti 3, 2024 katika Wilaya ya Mvomero na Kilosa Mkoani Humo ambapo anatarajia pamoja na miradi mingine atazindua kiwanda cha sukari cha Mkulazi kilichopo katika Wilaya ya Kilosa.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.