Na. Andrew Chimesela, Morogoro
Pamoja na changamoto zilizotaka kujitokeza wakati wa zoezi la upigaji kura, Mkoani Morogoro bado zoezi hilo limeendelea kuwa ni la Amani na utulivu huku Mkuu wa Mkoa huo Loata Ole Sanare akitoa wito kwa wananchi wake kufuata maagizo ya NEC ya kutokusanyika karibu na maeneo ya kupigia kura.
Loata Sanare ametoa wito huo leo mara baada ya kutimiza haki yake ya kikatiba ya kumchagua kiongozi ampendae kwa kupiga kura katika kituo alichojiandikisha cha Liti Chuoni.
Kwa kuwahakikishia wananchi Loata Sanare amesema amekwisha ongea na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya zote Mkoani humo na kuthibitishiwa kuwa hali ya Amani ni shwari na watu wameendelea na zoezi bila mashaka yoyote.
“Tunamshukuru Mungu tumeanza zoezi la Uchaguzi leo katika Mkoa wetu wa Morogoro na kwa kweli wananchi wameanza kwa wakati kwa asilimia kubwa na wengine wote sasa wameanza, Amani imeendelea kutamalaki kila mahali, nimeshaongea na Wakuu wa Wilaya wote wamenihabarisha kuwa hali ya Amani ni shwari” amesema Loata Sanare.
“wito wangu kwa wananchi wengine ambao hajatoka kwenda kupiga kura watoke wakapige kura, tutoke tukawachague viongozi tunaowataka. Leo ni siku ya kufanya uamuzi utakaotusaidia kwa miaka mingine mitano wenzetu wamepita huko kupiga kampeni sasa uamuzi ni wa kwako mwananchi” alisisitiza Loata Sanare.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa alitoa taarifa kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wasiopenda Amani katika Wilaya ya Ulanga Kata ya Minepa waliokuwa wanahamasisha wapiga kura kubaki eneo la kupigia kura mara baada ya zoezi hilo kinyume na maagizo ya NEC, hali ambayo ilithibitiwa na jeshi la polisi na wahusika kutoroka huku jeshi la polisi likiendelea kuwatafuta.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare alitembelea makundi maalum ikiwa ni pamoja na Wazee wa Kituo cha Funga funga kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuhakikisha endapo kundi hilo limepewa haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
Akiwa katika kituo hicho cha kutunzia wazee, alihakikishiwa na wazee hao akiwemo Mzee Joseph Paulo aliyesisitiza kuwa wamepatiwa haki yao ya msingi ya kwenda kupiga kura.
“kwa hakika wote tumekamilisha lengo lile la kwenda kupiga kura pale Railway Club bila kuguswa wala bila misukosuko ya aina yoyote”, alibainisha Mzee Paulo ambaye ni mmoja wa wazee wanaohifadhiwa katika kambi hiyo.
Akiongea na Waandishi wa Habari Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Morogoro Jocob Kayange amesema katika Mkoa mzima kuna vituo vya kupigia kura 4,774 na hadi anatoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari alikuwa hajapata changamoto yoyote iliyojitokeza.
Mkoa wa Morogoro una jumla ya Majimbo 11 ambayo yatawezesha kukamilisha zoezi la kuwapata Wabunge 11, una kata 214 zitakazowezesha kupatikana kwa Madiwani 214, ina idadi ya vituo vya kupigia kura 4,774 na wapiga kura waliojiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura ni 1,623,629.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.