Waziri Mkuu awasimamisha watumishi 7 Wilayani Kilombero
Na Andrew Chimesela - Ifakara
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi saba wa Halmashauri za Kilombero na Ifakara Mji Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro kwa tuhuma za ubadhilifu wa zaidi ya Tsh. 1.3 Bil. ambazo zinatokana na makusanyo ya mapato ya ndani.
Mhe. Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi hao leo (Jumapili, Septemba 15), mwaka huu wakati akiongea na watumishi wa Halmashauri hizo akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara Mkoani Morogoro.
Mbali na kuwasimamisha kazi watumishi hao, pia Waziri Mkuu ameagiza watumishi wote wanaotuhumiwa kurejesha fedha wanazotuhumiwa kuzichukua ndani ya siku tatu kabla hajamaliza ziara yake mkoani humo.
Watumishi wanaotuhumiwa na sakata hilo ni pamoja na Reina Mrema ambaye anadaiwa kuchukua kiasi cha sh. milioni 298, Haile Njitango milioni 73, Linus Mdembo kiasi cha sh. milioni 2 kwa kushirikiana na Gregory Midas ambaye ni mtendaji Kata wa viwanja Sitini katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Kuhusu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Francis Ndulane ambaye ametuthumiwa kuingiziwa fedha Serikali sh. milioni sita katika akaunti yake, Waziri Mkuu ameagiza fedha hizo zirudishwe mara moja huku akitakiwa kukabidhi stakabadhi ya marejesho hayo kwa Waziri Mkuu kabla hajamaliza ziara yake mkoani hapa.
Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) kipindi cha mwaka 2016 hadi juni 2019, Katika mji wa Ifakara makusanyo yalikuwa ni bilioni 2.7 ambapo fedha iliyopelekwa banki ni shilingi bilioni 1.9 na kufanya kiasi cha shilingi milioni 727 kutokuwa na maelezo ya kutosha ya matumizi yake.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameagiza Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Halmashauri ya Mji Ifakara John Mvanga kurejeshwa kazini mara moja, kulindwa, kutobughudhiwa na kuendelea kufanya kazi katika kituo chake cha awali.
Bw. Mvanga anaelezwa kuwa ndiye aliyeibua uwepo wa ubadhilifu wa fedha zilizotajwa hapo juu na badae kusimamishwa kazi. “Mlimsimamisha kazi kwa sababu mlijua amegundua madudu yenu, lakini haisaidi, arejeshwe kazini naagiza apewe ulinzi wa kutosha.” Alisisitiza Waziri Mkuu.
John Mvanga Mkuu wa Kitengoo cha TEHAMA aliyekuwa amesimamishwa kazi
Kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, Waziri Mkuu amesema zaidi ya sh. milioni 600 hazijulikani zilipo huku kiasi cha shilingi milioni 98.5 zikidaiwa kuingizwa katika akaunti za watumishi wa Halamshauri hiyo bila maelezo yeyote.
Watumishi wa Halmashauri za Kilombero na Ifakara Mji pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri hizo
Waziri Mkuu amewataja watumishi walioingiziwa fedha hizo ni pamoja na Devid Onyango aliyechukua kiasi cha milioni 51, Elakada Kanongole milioni 36, Fork Karunde milioni 8 na Charlse Chali milioni 2.5.
Waziri Mkuu akiongea na Watumishi
Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na kuongea na Watumishi wa Halmashauri hizo mbili za Kilombero na Ifakara Mji pia aliongea na wananchi wa Mchombe na Mlimba katika Halmashauri ya Kilombero na kesho anatarajia kuendelea na ziara yake katika Halmashauri za Malinyi na Ulanga.
MWISHO
|
|
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.