Waziri Mkuu ataka wananchi washirikishwe kilimo cha miwa shamba la Mkulazi II
Na. Andrew Chimesela – Morogoro
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema uwepo wa shamba la miwa la Mkulazi II utowe fursa kwa wananchi wa maeneo jirani kulima zao hilo ili kuwaongezea kipato wananchi hao na hivyo kujikwamua na umaskini.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Disemba 7 mwaka huu wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani Morogoro aliyoifanya kwa lengo la kutembelea shamba hilo la miwa ambalo liko Mbigiri katika Wilaya ya Kilosa.
Waziri Mkuu amesema Mkakati wa Serikali katika kukuza kilimo cha miwa na kuzalisha sukari kwa wingi imedhamiria pia kuhusisha wakulima wadogo wanaozunguka eneo lote la Mkulazi II. Amesema baada ya kutenga eneo lilnalotakiwa kulimwa pembeni yake lazima wahusishwe wakulima wadogo kusaidia kuzalisha miwa kwa ajili ya kiwanda hicho.
“Tulishanunua matrekta ambayo tulitarajia wananchi wale wangelimiwa na matrekta ya Serikali hawakufanya hivyo, kwa hiyo naamini nyie mtafanya hivyo”. Amesema Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka Bodi zote mbili zinazoendesha shamba la Mkulazi II kuhakikisha shamba hilo linakuwa la mfano kwa mashamba mengine ya miwa hapa nchini kwa kuwa Serikali ina wataalamu wa kutosha na wenye weledi.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema Bodi ya Mkulazi na Bodi ya NSSF zimejizatiti kuona kuwa mradi huo unatekelezeka bila ya kipingamizi.
Hata hivyo Jenista amezitaka Bodi hizo kuwa na Uzalendo, maadili ya utendaji kazi na uaminifu ili mwisho mradi huo wa kilimo cha miwa ulete tija sio kwa taifa tu lakini pia kurejesha fedha za wanachama wake na kukuza uchumi wa nchi.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amemuomba Waziri Mkuu kusaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha Sukari cha Mkulazi I kuanza uzalishaji wake mapema, huku Mkuu wa Mkoa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe akitumia fursa hiyo Kumuomba Waziri Mkuu kuanzisha kituo cha kuuzia zao la korosho katika Mkoa wa Morogoro.
DKT. Kebwe amesema, Msimu huu Mkoa wa Morogoro umevuna korosho tani zaidi ya elfu tano, huku Halmashauri zote za Wilaya za Mkoa huo zimejipanga kulima zao la Korosho hivyo kuna umuhim wa kuwa na kituo hicho cha kununulia korosho.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya Mkulanzi Holding Company Dkt. Hildelitha Msita ametaja baadhi ya changamoto za shamba la miwa la Mkulazi II kuwa ni pamoja na kukosekana kwa miundombinu ya umeme, kutokuwa na uhakika wa mashine za kiwanda na ukosefu wa miundombinu ya umwagiliaji.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.