Dkt. Kebwe awataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi kujipanga
Na. Andrew Chimesela - Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Mkoa huo kujipanga katika kutoa Elimu na kuhamasisha wananchi hususan Wajasiliamali wadogo kuwa na vitambulisho vya kufanyia Biashara zao na kwamba hicho kitakuwa moja ya kigezo cha utendaji kazi wao.
Dkt. Kebwe ametoa kauli hiyo Februari 4 mwaka huu wakati wa kikao cha tathmini na kujiwekea mikakati ya kuongeza kasi ya uuzaji wa vitambulisho vya wajasiliamali wadogo ambacho kilishirikisha Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo.
Akifunga kikao hicho ambacho pia kilikuwa ni cha kushirikishana na kupeana mbinu za kufanikisha zoezi hilo la utoaji wa vitambulisho kwa wajasiliamali wadogo, Dkt. Kebwe alisema utekelezaji wa zoezi hilo kwa viongozi litakuwa ni moja ya vigezo katika utendaji wao wa kazi.
“sisi viongozi, vigezo viwili tu, vitambulisho na kusimamia mapato ya makusanyo kwenye Halmashauri zetu, kwa hiyo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi kigezo hiki kilichoongezeka kitatathmini uwezo wa ninyi viongozi..”alisema Dkt. Kebwe.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa muda hadi Februari 28 mwaka huu, kila Mkuu wa Wilaya awe amehamasisha wajasiliamali wadogo kununua vitambulisho hivyo kwani wajasiliamali wengi wanavihitaji isipokuwa wanahitaji kuongozwa mahali pa kuvipata.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Clifford Tandari ambaye kimsingi ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali ngazi ya Mkoa amewataka Viongozi na Watumishi wote wa Serikali Mkoa humo kufanya kazi kwa Kushirikiana badala ya Kushindana.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Seriel Mchembe aliwatoa hofu Viongozi wa Kisiasa ngazi za Wilaya Wakiwemo Wahe. Madiwani kuwa, zoezi la wajasiliamali wadogo kulipa kodi Serikali Kuu halilengi kupunguza mapato ndani ya Halmashauri bali kuongeza mapato hayo.
Kikao hicho kimekuja baada ya kuwepo kwa kasi ndogo ya uuzaji wa vitambulisho hivyo kwa walengwa ambapo hadi kufikia Januari, 27 mwaka huu Mkoa wa Morogoro ulikuwa umeuza vitambulisho 3,764 tu sawa na 15.056%.na kuwataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuongeza kasi ya uuzaji huo wa vitambulisho.
Katika Kikao hicho imeamriwa kuwa kila mfanyabiashara kwenye sekta isiyo rasmi asiruhusiwe kufanya biashara yake bila kuwa na kitambulisho kinachomruhusu kufanya biashara kama hajalia kodi TRA, ama Halmashauri, ama awe na kitambulisho cha Mjasiliamali mdogo.
MKoa wa Morogoro awali ulipata jumla ya vitambulisho 25,000 na awamu hii ya pili imepata jumla ya vitambulisho 40,000 ambavyo Mkuu wa Mkoa amevigawa tayri kwa Wakuu wa Wilaya na kufanya Mkoa mzima kuwa na vitambulisho 65,000.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.