Tanzania kuendelea kunufaika Kiuchumi ndani ya SADC
Na Andrew Chimesela - Morogoro
Imeelezwa kuwa Tanzaina inanufaika kiuchumi kama mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na jumuiya nyingine ambazo Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya hiyo.
Hayo yameelezwa leo Julai 9 na Katibu Mkuu Mstaafu Ofisi ya Waziri Mkuu, Mussa Uledi wakati akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya waandishi wa habari ya kuwajengea uwezo wa kuandika na kuripoti habari za SADC,ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo hayo yanayofanyika siku tatu Mkoani Morogoro.
Bw. Uledi amesema Tanzania imenufaika na utekelezaji wa miradi ya miundomnbinu, biashara, uwekezaji na viwanda.“ Mkakati wa maendeleo wa SADC unafafanana kwa kiwango kikubwa na ule wa Tanzania ambao pia unazingatia haja ya utekelezaji wa viwanda na miundombinu hapa nchini hali itakayochangia katika kuimarisha maendeleo na kukuza uchuni na ustawi wa wananchi” Alisisitiza Bw. Uledi.
Akifafanua Zaidi amesema kuwa vipaumbele vya Tanzania vimejikita katika upanuzi wa Mauzo nje na uongezaji wa michepuo yake lengo likiwa ni kukuza na kuendeleza biashara hali inayowezesha uendelezaji wa viwanda vya kuongeza thamani katika malighafi za ndani hususan mazao ya kilimo na madini.
Aliongeza kuwa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli katika baadhi ya nchi wanachama wa SADC imeonesha kuwa Tanzania imejipanga vizuri kimkakati na inaweza kuwa ghala la Chakula kwa kukuza Zaidi uzalishaji kuendana na mahitaji katika soko la jumuiya na hata nje ya jumuiya hiyo.
Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na uendelezaji miundombinu kama barabara, reli, usafiri wa anga, uzalishaji na usambazaji huduma za umeme ambayo ni nyenzo muhimu sana katika kuyaunganisha masoko ya nchi wanachama wa SADC.
Aliongeza kuwa vipaumbele vingine ni utafutaji wa rasilimali na utekelezaji wa miradi ya Kikanda kwa kuundwa kwa kikosi kazi cha Mawaziri wenye dhamana ya Fedha na uendelezaji miundombinu, Amani na Usalama umeendelea kuimarika ndani ya SADC.
Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Brigedi ya Magharibi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kanali Wilbert Ibuge akiwasilisha mada katika mafunzo hayo ambayo kesho Julai 10 yanafikia hatima yake kwa awamu ya kwanza amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa Barani Afrika zilizotoa mchango mkubwa na kuratibu kuanzishwa kwa Jumuiya ya SADC.
Aidha amewahakikishia watanzania kuwa hali ya amani na usalama kwa sasa imeendelea kuimarika katika SADC kama inavyojidhihirisha kwa takribani nchi zote za SADC ambapo nchi wanachama ziliazimia kusimamia maendeleo ya kiuchumi ya Kanda kwa kuzingatia malengo ikiwemo kukuza uchumi, kuondoa umasikini, kuboresha hali ya maisha ya wananchi kutoka nchi wananchama.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.