Morogoro wafanya kumbukizi ya wahanga wa ajali ya Moto
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare leo Agosti 10, 2020 ameungana na ndugu Jamaa na marafiki wa wahanga wa ajali ya moto uliotokea kutokana na Lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto Agosti 10 mwaka jana na kusababisha vifo vya watu 115 katika eneo la Msamvu Mkoani hapa.
Akihutubia wananchi waliofika eneo la makaburi ya Kola wakati wa kumbukizi tukio hilo, Loata Sanare pamoja na kutoa pole kwa ndugu, kwa kuwapoteza wapendwa wao, amewataka wananchi kujijengea utamaduni wa kutoa mapema taarifa za majanga ya moto ili kuokoa maisha ya watu na mali zao kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akiweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu wa makaburi ya wahanga wa moto Kola Mjini Morogoro
Mkuu huyo wa Mkoa pia ameiagiza Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Morogoro kuratibu na kusimamia majanga kama hayo yasitokee na kusababisha maafa makubwa kama ilivyotokea katika ajali hiyo ya moto badala yake hatua zichukuliwe mapema.
“Aidha, naiagiza Kamati ya maafa ya Wilaya kuendelea kusimamia na kuratibu mpango wa kuzuia majanga na kuchukua hatua ya kukabiliana nayo pindi yanapojitokeza” alisema Sanare
Pamoja na agizo hilo, Loata Sanare amewataka wamiliki wa magari makubwa ya mizigo kupanga ratiba za madereva wa magari hayo kuwa zaidi ya mmoja ili kupokezana mara mmoja wao anapochoka kuendesha ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Katika hatua nyingine amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wakishirikiana na Kamati inayojenga Makaburi ya wapendwa waliopoteza maisha katika ajali ya moto kuhakikisha ujenzi wa makaburi hayo unakamilika kwa wakati na kwa ubora kama maagizo ya Waziri Mkuu yalivyotolewa.
DC Morogoro naye akiweka shada la maua
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa amewataka wananchi kujiepusha na tabia ya kusogea eneo ambapo magari yamepata ajali kwa nia ovu hususan magari ya mizigo yaliyobeba mafuta, sumu au mizigo mingine hatari ili kujinusuru na janga lolote linaloweza kujitokeza katikaeneo hilo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo (mwenye suti nyeusi picha ya juu na chini) na Sheilla Lukuba Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa ya Manispaa ya Morogoro wakiweka mashada
Kwa upande wao jeshi la zimamoto na uokoaji wamewataka wananchi kutoa mapema taarifa za kweli kwa jeshi hilo kupitia namba ya dharura na uokoaji 114 ambayo mwananchi halipishwi, lengo ni kulifanya jeshi hilo kufika eneo la ajali kwa wakati na kuokoa maisha ya watu na mali zao.
Kamanda wa jeshi la ziamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro Goodluck Zelothe, akimkabidhi kizimia moto Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ishara ya kuwataka wananchi wote Moani humo kuwa na vizimia moto kwenye makazi yao ili kujiokoa na majanga ya moto pindi yanapotokea.
Akiongea kwa niaba ya ndugu wa marehemu Bw. Alli Ramadhani Muhenge aliwashukuru viongozi wote wa Serikali wakiongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada za kushiriki kikamilifu wakati wa janga la moto lilipotokea, lakini pia kwa kuwahifadhi marehemu wao kwa kuwajengea makaburi na mnara wa kumbukumbu.
Waombolezaji
Kwa Mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba amesema katika ajali hiyo watu 115 walipoteza maisha wanaume wakiwa 109 na wanawake 6 na kuasbabisha majeruhi 21 wanaume wakiwa 16 na wanawake 5.
Baadhi ya majina ya watu waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea Agosti 10, 2019
Kufanyika kwa kumbukizi hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeagiza kuwakumbuka wahanga hao kila inapofika tarehe 10 ya mwezi Agosti ya kila mwaka.
Huu ndi mnara wa kumbukumbu uliojengwa kwenye makaburi ya wahanga wa moto katika makaburi ya Kola - Morogoro. Wapumzike kwa Amani Amen
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.