Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amewataka wamiliki wa viwanda Mkoa wa Morogoro kushiriki maonesho ya tano ya bidhaa za viwanda Tanzania ili kupanua ujuzi katika kuendesha viwanda hivyo na kutumia fursa ya kukutana na wamiliki na wenye viwanda kutoka mikoa mingine wakati wa maonesho hayo.
Hayo yamebainishwa Oktoba 9 mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kwenye kikao cha kujadili ustawi wa maendeleo ya viwanda mkoani humo, uliokutanisha wamiliki wa viwanda kwa Mkoa huo na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade Boniface Michael (wa pili kulia) katika kikao cha kujadili ustawi wa maendeleo ya viwanda Mkoani Morogoro kilichofanyoka katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Loata amesema uwekezaji kwenye viwanda umepewa kipaumbele na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dr. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo utekelezaji wa sera ya maendeleo endelevu ya viwanda ya mwaka 1996 –2020 imelenga kuiwezesha sekta ya viwanda kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu kama ilivyoainishwa katika dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.
Pia, amewasisitiza wawekezaji kuanzisha viwanda hususan viwanda vidogo vya kusindika mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kupanua wigo wa ajira kwa wananchi na huku akiwaagiza Wakuu wa Wilaya katika Mkoa wake kuhakikisha wanajadili changamoto wanazokumbana nazo juu ya uwekezaji ili kuboresha uwekezaji katika Wilaya zao.
“Natumia fursa hii kuwahimiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba vikao vya wawekezaji kwenye viwanda na maeneo mengine, viwe vinafanyika mara nyingi ili kujadili changamoto za wawekezaji na kuboresha uwekezaji kwenye Wilaya zetu. Pia, nawahimiza Wawekezaji kuendelea kuhamasisha uanzishaji wa viwanda, hususan vidogo vidogo vya kusindika mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kupanua wigo wa ajira kwa wananchi wetu” alisema Loata
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya (wa kwanza kushoto),wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya Kilombero Sacp Ismail Mlawa ,wengine ni baadhi ya wamiliki wa Viwanda waliohudhuria katika Kikao hicho.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema ushiriki wa wamiliki wa viwanda utawasaidia kutangaza biashara zao na kuona wafanyabiashara wengine wanavyoendesha kazi zao kwa biashara zile zile na kutambua namna ambavyo watafanya maboresho katika bidhaa hizo ili kusaidia kukuza soko la bidhaa katika mkoa wa Morogoro.
Aidha, Mhandisi Kalobelo ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzisha jengo (One Stop Centre) ambalo litakuwa na wataalamu wote watakaokuwa pamoja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuondoa kero kwa kwao wanapofuatilia masuala mbalimbali ya kuanzisha uwekezaji ndani ya Mkoani.
Vile vile Mhandisi Kalobelo amechukua nafasi hiyo kuwaagiza wakuu wa Wilaya mkoani humo kuhamasisha Halmashauri kutenga maeneo kuanzia ngazi ya vijiji na kata kwa ajili ya uanzishwaji wa viwanda ili kuwasaidia wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vidogo vidogo kupata sehemu yao maalumu kwa ajili ya kazi zao.
“Tunaanzisha utitiri wa viwanda ndani ya maeneo ya Makazi, lakini ardhi zipo tusifanye ardhi kuwa gharama kubwa yani Halmashauri zisitumie ardhi hii inayotengwa kwa ajili ya viwanda kama chanzo cha mapato tena hapa tunawezesha ili kuandaa walipa ushuru na kodi katika maeneo yale” alisisitiza Kalobelo
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade Boniface Michael, amewaeleza wamiliki wa viwanda Mkoa wa Morogoro kutumia jukwaa la Maonesho ya tano ya bidhaa za viwanda ili kupanua wigo wa masoko nje ya Mkoa wa Morogoro na kuwatambulisha watanzania bidhaa wanazozalisha ili kuchochea uzalishaji, kuwaunganisha wenye viwanda na wazalishaji mbalimbali wa mali ghafi na huduma zingine zinazotumika viwandani.
Maonesho haya ya tano ya Bidhaa za Viwanda yanatarajiwa kufanyika Novemba 3 hadi 9 mwaka huu katika viwanja vya maonesho ya Mwl J.K.Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ambapo Mikoa mbalimbali hapa nchini itashiriki.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.