RC Morogoro awajia juu Watendaji Kata, Kamati za Maendelo Kata.
Na Andrew Chimesela - Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameuagiza Uongozi wa Kata ya Magadu na Kata ya Mbuyuni katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kutumia fedha zilizoletwa na Serikali ndani ya miezi miwili badala ya kuendeleza malumbano na kusababisha fedha hiyo kukaa kwa muda mrefu.
Loata Sanare ametoa agizo hilo Juni 30, 2020 alipotembelea shule ya Sekondari ya SUA na kukutana na Wajumbe wa Kamati za Baraza la Maendeleo Kata ya Mbuyuni na Kata ya Magadu ambazo kila Kata inaamini kuwa shule hiyo iko katika eneo lake.
Mkuu wa Mkoa amelazimika kufika katika shule ya Sekondari ya SUA na kufanya kikao hicho kutokana na kamati hizo kushindwa kuzitumia fedha shilingi milioni 39 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga madarasa mawili, kutokana na kuwepo kwa malumbano hayo huku kila Kata ikidai fedha hiyo iingiziwe kwenye akaunti ya Kata yake.
Katika Kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ametoa miezi miwili kwa fedha hiyo kufanya kazi iliyokusudiwa kwani haoni sababu ya malumbano hayo ambayo kimsingi yanachelewesha fedha ya Serikali kufanya kazi iliyokusudiwa.
“huyo anayesema kwa nini utume magadu, kwa nini tume Mbuyuni sasa mnagombania nini shule ni hiyo hiyo moja, au ulitaka Mbuyuni iwe ya kwako uweze kufanya mambo yako, au ulitaka fedha ziingie magadu uweze kufanya unayoyataka, kwa sababu mimi sioni tatizo” amesema Loata Sanare.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare (mwenye suti) akitembelea mazingira ya shule ya Sekondari ya SUA kabla ya kuanza kikao
zaidi Sanare amewaonya Watendaji wa Kata ya Magadu na Mbuyuni na wajumbe wengine ndani ya Kata hizo kwa uzembe uliofanyika ambao uligubikwa na maslahi binafsi huku akionya kuwa yeyote atakayegusa fedha hiyo ya Serikali atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Katika hatua nyingine, Sanare ameitaka Bodi ya shule ya Sekondari ya SUA kwa kipindi hiki ambapo bado kuna ugonjwa wa CORONA kutafuta uwezekano wa wanafunzi kukaa kwa nafasi wakisubiri madarasa mawili yanayojengwa na kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula kwani kuna muda mrefu kwa wanafunzi kuwepo shuleni.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Mbuyuni wakisikiliza kwa makini maagizo ya Mkuu wa Mkoa
Aidha, kupitia walimu wa Sekondari ya SUA Sanare amewataka walimu wote Mkoani Morogoro kujituma katika kufanya kazi zao na kufuata taratibu na miongozo yote iliyotolewa na Serikali kupitia Wiazara husika huku akiwataka kuongeza juhudi katika kuinua matokeo ya mitihani katika shule wanazofundisha.
Kuhusu mipaka, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kutambua mipaka ya shule hiyo ili kujua shule hiyo kwa sasa iko Kata gani na Kata itakayoonekana haina shule ya Sekondari iweke mikakati ya kuanza kujenga ili kutekeleza agizo la Serikali la Kata kuwa na shule ya Sekondari
Katika kikao hicho, walimu wa Sekondari ya SUA walitoa mapendekezo yao ya kubadili mfumo wa utoaji wa fedha Serikali kwenda kwenye taasisi, kwani mfumo wa sasa unasababisha migogoro mingi baina ya Madiwani na Wakuu wa Taasisi zinazolengwa kupewa fedha hizo.
Baadhi ya Walimu wa shule ya Sekondari ya SUA wakifurahia maamuzi ya kikao hicho hususan ujenzi wa Jengo la Utawala ambalo litawapa mazingira mazuri kwa kazi zao
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba amesema amesikitishwa na mgogoro huo na kuahidi kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha Ofisi yake itaanza kupeleka fedha lengwa moja kwa moja kwenye Taasisi husika bila kupitia akaunti za Kata ili kuepusha migogoro kama hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akiwapa zawadi ya fedha wanafunzi wawili wa shule ya Sekondari ya SUA baada ya kujibu vizuri namna ya kujikinga na ugonjwa wa CORONA
Mkuu wa shule, Sekondari ya SUA Bw. Festo Kayombo alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa pamoja na fedha hizo kulenga kujenga madarasa mawili na kutengeneza viti na meza kwa ajili ya wanafunzi, shule imeomba imeomba kubadili matumizi ya fedha hizo zikarabati madarasa mawili yaliyokuwa yanatumika na walimu kama Ofisi ili fedha zitakazobaki zijenge Jengo la Utawala ambalo ni hitaji muhim kwa sasa katika shule yao.
moja ya majengo ya Shule ya Sekondari ya SUA
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.