RC MOROGORO ATAMANI KUONANA NA MAASKOFU.
Na Andrew Chimesela – Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameonesha dhamira ya kutaka kuonana na wamiliki wa shule ya Seminari ya Mtakatifu Petro ya Mkoani hapa inayomilikiwa na Kanisa Katoliki ili kueleza dhamira yake ya kutaka kuifunga shule hiyo kutokana na uwepo wa miundombinu chakavu pamoja na shule hiyo kutokuwa na Bodi inayokidhi vigenzo vya Serikali.
Loata Sanare ametoa kauli hiyo Juni 20 mwaka huu alipofanya ziara ya kushtukiza katika Seminari hiyo, baada ya kupata taarifa kuwepo kwa mapungufu kuwa shule hiyo ina miundombinu chakavu na kuna migogoro ya kimahusiano baina ya uongozi wa Shule na wafanyakazi wa shule hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare (mwenye suti nyeusi) akiangalia ndoo ya maji kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo kunawa mara watakapofungua shule ikiwa ni moja ya tahadhari ya kujiepusha na ugonjwa wa CORONA. kulia kwa Mhe. Sanare ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo.
Imeelezwa kuwa hali hiyo ya kuwepo changamoto ambazo hazina majibu kwa muda mrefu inatokana na shule hiyo kukosa Bodi ya shule ambayo inakidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali.Kwa sababu hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amefika shuleni hapo ili kujiridhisha hali ya miundombinu pamoja na kusikiliza kero chache kutoka kwa wafanyakazi na baada ya hayo akatoa tamko la kutaka kuonana na mmiliki wa shule ambao ni Maaskofu wanaomiliki shule hiyo ili kuwaeleza dhamira ya kutaka kuifunga shule hiyo endapo mapungufu yaliyopo hayatarekebishwa kwa wakati.
“shule haina Bodi nataka niwaambie hilo, na kama haina bodi hakuna mamlaka ya kuitwa shule….mimi nitafurahi kuonana na wamiliki wa shule ambao ni maaskofu na kuwaambia dhamira yangu ya kutaka kuifunga shule kama haitarekebishwa” alisema Loata Sanare.
Aidha, Sanare alimuagiza Mkuu wa shule hiyo kufuata miongozo ya Serikali katika uendeshaji wake na kwamba hata kama shule hiyo ni ya Binafsi ni lazima ifuate wa Serikali ikiwa ni pamoja na utendaji kazi wa bodi ya shule hiyo uwe wazi na upitie Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.Katika hatua nyingine Loata Sanare ameitaka Bodi ya shule iliyopo ikutane mara moja na kutembelea mazingira yote ya shule ili kuona na kupendekeza kwa wamiliki jambo la kufanya kwa lengo la kuboresha mazingira ya shule hiyo.
RC Morogoro akitembelea mazingira ya shule ya Mt. Petro iliyopo Mkoani humo. Katikati ni Gombera wa shule hiyo Fr. Aloyce Mwenyasi
Amesema shule hiyo ina heshima yake tofauti na shule nyingine, kwanza ni shule inayomilikiwa na Maaskofu, lakini pili, inaongozwa na Mapadre na Masista hivyo hangependa yawepo manung’uniko yoyote zaidi ya kuwa ni shule ya mfano.Nao wafanyakazi wa shule hiyo akiwemo Charles Mabiki na Isack Petro waliowawakilisha wenzao, wamesema shule hiyo ina changamoto nyingi, zikiwemo za kimahusiano yasiyoridhisha na uchakavu wa miundombinu ambapo pamoja na kutoa ushauri namna ya kuzitatua lakini ushauri wao umekuwa haufanyiwi kazi.
Baadhi ya Watumishi wa shule ya Mt. Petro wakitoa kero zao wakati Mkuu wa Mkoa alipotembelea shule hiyo.
Aidha, wamesema shule hiyo ina walimu vijana wengi ambao bado wana ari ya kufanya kazi na ndio maana shule hiyo imekuwa ikitoa matokeo mazuri kwenye mitihani na hata kuingia kwenye kumi bora, lakini wanakatishwa tamaa na changamoto ambzo hazipewi kipaumbele katika kuzitatua huku zikiwa na athari kwa afya yao na wanafunzi. Kwa upande wake Gombera (Mkuu wa shule) hiyo Padre Aloyce Mwenyasi wa jimbo la Morogoro, amekiri kuwa shule hiyo kwa sasa ina miundombinu iliyochakaa kwa kuwa ukarabati wa mwisho ulifanyika miaka 25 iliyopita hivyo unahitajika ukarabati mwingine na kwamba atawasilisha ujumbe huo kwa maaskofu ili waweze kuyafanyia kazi maagizo aliyotoa Mkuu wa Mkoa.
Shule ya Mtakatifu Petro ni shule ya kikatoliki na lengo la kutoa Elimu ya Sekondari kwa vijana Wakatoliki wanaotaka kuwa mapadre wa baadae mbapo kwa sasa shule hiyo ina ina jumla ya wanafunzi 357.Shule hii inayojulikana zaidi kwa jina la St. Peter Seminary, ilianzishwa mwaka 1937 huko Ilonga Wilayani Kilosa, mwaka 1939 ilihamishiwa Bagamoyo na miaka 30 baadae ilihamishiwa hapa Morogoro mjini. Kwa sasa shule inamilikiwa na Maaskofu wa Kanisa Katoliki wa majimbo tisa (9) ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Mahenge, Dodoma, Zanzibar, Kondoa, Ifakara na Same.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.