RC Morogoro aagiza aliyemshambulia Mwalimu akamatwe
Na Andrew Chimesela - Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameagiza Jeshi la Polisi Mkoani humo kumkamata mara moja Bw. Maluhanga Lutwele kwa tuhuma za kumshambulia na kitu chenye ncha kali Mwalimu Mohamed Mstapha Mjema wa shule ya Sekondari Mela baada ya kuzuia mifugo wake wasichunge ndani ya eneo la shule hiyo.
Loata Ole Sanare ametoa agizo hilo Agosti 4 mwaka huu alipofika katika Shule ya Mela iliyopo Wilayani Mvomero Mkoani humo kwa lengo la kutoa pole kwa walimu wa shule hiyo na kuwahakikishia kuwa Serikali ipo pamoja nao katika tukio hilo ambalo ameliita ni la kihuni na kwamba aliyefanya kitendo hicho lazima akamatwe.
“Niwatie moyo kwamba Serikali ipo na ninyi, hili jambo si dogo katika mambo ambayo nitayashikia bango kwa nguvu zangu zote ni pamoja na hili, ni lazima mtu huyu akamatwe apelekwe kwenye vyombo vya sheria, na kwa kweli lazima abebe msalaba wake” aliagiza Loata Sanare.
Sambamba na maagizo hayo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare amemwagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Mela Tobiko Letika eneo lilipotokea tukio hilo kuandaa Mkutano wa viongozi wa kijiji hicho ambao wengi ni jamii ya kifugaji (Leigwanani) ili kufanya nao mkutano wiki lijalo.
“Lazima tuwakamate hawa, lazima. haiwezekani wakafanya upuuzi tukawaacha, kwa hiyo nakuachia nitafutie maleigwanani wote hata wa majirani wa kata hizi sio lazima wa kata ya Mela pekee..”. alisisitiza Loata Sanare.
Amesema Serikali haitawaacha salama watu wanaojihusisha na matukio ya kuwashambaulia walimu ambao wametumwa na Serikali na wanalipwa mishahara na Serikali kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao na kisha wafanyiwe vitendo visivyofaa.
Akisisitiza juu ya kukamatwa kwa mtuhumiwa Lutwele, amemtaka Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mvomero kumkamata mtuhumiwa huyo huku akiitaka familia ya kijana huyo kuwajibika kwa kitendo alichofanya kijana wao katika kununua miti iliyoharibiwa na mifugo yao katika eneo la shule ya Mela, kuinunua kwa gharama zao, kuipanda na kuimwagilia kwa kuwa mifugo hao ni wa familia na sio wa kijana huyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mela Tobiko Letika amesema kitendo hicho kimewakasirisha na kuwasikitisha sana na kinawaharibia sifa yao, hata hivyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwakimbilia katika tukio hilo huku akiahidi kwa kushirikiana na wananchi wake kukomesha mara moja vitendo hivyo visitokee tena kijijini hapo.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mela Bi. Sophia Mwafyuma amesema, tukio hilo limeleta simanzi kwa walimu wake na wanafunzi kushindwa kusoma. Amesema, hilo sio la tukio la kwanza, yamewahi kutokea matukio mengine siku za nyuma bila kushughulikiwa na hata wanafunzi wake waliwahi kunusulika kubakwa majira ya usiku baada ya watu wasiofahamika kutaka kuvunja milango, hivyo kwa sasa hawana utulivu katika masomo yao.
Ameongeza kuwa baada ya tukio hili, walimu wengi katika shule yake wameanza kufanya taratibu za kiutumishi kutaka kuhama shuleni hapo kwa madai kwamba usalama wao na mali zao viko hatarini.
Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Mela akiwemo Kandai Mtemi, Mambega Almasi, na Saito mwalimu wameonekana kusikitishwa na tukio la kupigwa Mwalimu wao na mwananchi mwenzao Bw, Lutwele na kwamba kitendo hicho kimewadhalilisha huku wakiomba msamaha na kutaka sheria ichukue mkondo wake dhidi ya mhusika.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho ambapo shule ya Sekondari Mela ipo Oldani Mbulati naye amemwomba Mkuu wa Mkoa aangalie njia yoyote itakayowashawishi wananchi wa eneo hilo kufanya mchango wa fedha ili kujenga uzio wa shule hiyo na kukomesha changamoto hiyo na hali itakayowafanya wanafunzi kusoma kwa utulivu na walimu kuwa na amani katika kuwafundisha watoto wao.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mkuu wa shule hiyo mtuhumiwa Lutwele inasadikika alipeleka mifugo hao shuleni hapo Agosti 2 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni kwa ajili ya ng’ombe wake kupata malisho ndani ya eneo la shule hiyo. Mwl. Mohamed Mstapha Mjema aliwashikilia ng’ombe hao hadi majira ya saa moja jioni.
Na ilipofika mida kama ya saa mbili jioni Lutwele alifika shuleni hapo kwa ajili ya kuwachukua mifugo wake, alipoulizwa kwa nini amefanya jambo hilo alitoa majibu ambayo hayakuwa ya kiungwana ndipo yalipoanza majibizano yaliyopelekea mwalimu Mjema kushambuliwa kwa fimbo na kitu chenye ncha kali kichwani, mikononi na mgongoni na kuvuja damu nyingi na baadae kupelekwa katika kituo cha Afya cha Melela kwa ajili ya matibabu.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.