RC Morogoro akemea wanafunzi kubaguliwa
Na. Andrew Chimesela, Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amekemea Watendaji wa Serikali Mkoani humo kwa kutowajibika ipasavyo kwa kuruhusu wanafunzi katika baadhi ya shule za Msingi kupata chakula cha mchana shuleni huku baadhi yao wakiwa wamefungiwa ndani ya madarasani kwa kisingizio cha wazazi au walezi wao kutotoa michango ya chakula na kuagiza kuwa kitendo hicho kisirudiwe tena kwa kuwa ni kitendo cha kibaguzi.
Loata Sanare ametoa maagizo hayo Aprili 27 mwaka huu wakati wa hafla fupi ya kupokea msaada wa bati kwa ajili ya ukarabati wa madarasa ya shule ya Msingi ya Mji Mkuu iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambayo majengo yake yanahitaji ukarabati mkubwa ili wanafunzi wanaotumia majengo hayo kuwa na mazingira bora ya kusomea.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare (katikati) akipokea msaada wa bati 100 kutoka kwa mdau wa maendeleo Mchungaji Jerry Wyatt wa Kanisa la Faith Baptist. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo.
Amesema kuna baadhi ya shule za msingi ambapo walimu wao pamoja na Watendaji wa wengine wa Serikali wakiwemo Watendaji wa Kata kuacha wanafunzi kutoka baadhi ya shule kupata chakula cha mchana huku wanafunzi wengine wakiwa wamefungiwa ndani ya madarasa kitendo ambacho amekiita kuwa ni cha kinyama.
Amesema, haiwezekani watoto wengine wanakula chakula na wengine wanafungiwa ndani ya madarasa jambo linaloonesha kuwa viongozi wa eneo hilo hawafanyi kazi inavyopaswa kwani moja ya wajibu wao ni kuhakikisha wazazi wote wanachangia kama walivyokubaliana kwenye vikao vya kupanga michango hiyo baada ya kupata kibali cha Mkuu wa Wilaya na kutaka kitendo kisirudiwe tena.
“Lakini suala la watoto wachache kula chakula wengine wanafungiwa madarasani huo ni unyama ambao haukubaliki” alisema Sanare.
“Hili nalielekeza lisije likajirudia kabisa, ni mbaya, watoto huwezi kuwafungia darasani ni vizuri mkakusanya kadri mtakavyoweza , mkapika chakula kidogo kwa ajili ya watoto wote” alisistiza.
yanayoonekana kwa mbele ni majengo ya vyumba vya madarasa vinavyotakiwa kukarabatiwa ikiwa ni pamoja na kuezeka bati mpya
Naye Katibu Tawala wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kusema neno kwenye hafla hiyo alisema anapongeza jitihada zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa za kuboresha Elimu ndani ya Mkoa huo na kwamba kazi yake kiutendaji inakuwa nyepesi.
Aidha, Mhandisi Kobelo amesema ili kuhakikisha anakwenda na kasi ya Mkuu wake wa kazi, wajibu wake mkubwa ni kuhakikisha anaimarisha Kamati za shule za Msingi na Bodi za shule kwa upande wa shule za Sekondari ili wajue wajibu wao kikamilifu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare na Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo wakisaidiana na mafundi katika kupandisha kenchi kwenye moaj ya chumba cha Darasa la shule ya Msingi Mji Mkuu, walipofika hapo kwa ajili kupokea msaada wa bati 100.
Amesema inawezekana Bodi na Kamati hizo hazijaelewa kwa kina wajibu wao, hivyo anachokifanya sasa ni kuziwezesha kutambue wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi katika shule wanazozisimamia wanakuwa katika mazingira mazuri ya kujifunzia kitu ambacho anaendelea kukifanya.
Kwa upande wake Mdau aliyetoa msaada bati bati 100 zenye uwezo wa geji 28 kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo, Mchungaji Jerry Wyatt wa Kanisa la Faith Baptist lililopo Kola B katika Manispaa ya Morogoro, amesema yupo hapa nchini kwa muda mrefu kama Mchungaji ameguswa na mazingira yasiyo salama kwa wananfunzi hao na kuamua kutoa msaada huo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba (watatu kulia) akionekana kumshukuru Mchungaji Jerry Wyatt kwa msaada alioutoa.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.