Agizo la Rais la kuwajengea vibanda Wafanyabiashara laanza kutekelezwa
Na. Andrew Chimesela - Morogoro
Ni takriban siku mbili tu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutoa agizo la kutaka wafanya biashara wa eneo la Dumila maarufu kama Feli, ambao wako kandokando ya Barabara ya Dodoma - Morogoro kujengewa vibanda vya kufanyia biashara zao, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro imeanza kutekeleza agizo hilo la Rais.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akila mhindi wa kuchom mara tu alipowasili eneo la Dumila ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais. Bidhaa hiyo ni moja ya bidhaa zinazopatikana eneo la Dumila maarufu kama Feli ambapo Mhe Rais aliagiza wafanya biashara hao wajengewe vibanda vya kufanyia biashara zao.
Hatua hiyo imethihirika Agosti 6 mwaka huu, baada ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo pamoja na timu yake kufika eneo la Dumila kwa ajili ya utekelezaji wa agizo la Rais kwa kufanya Tathmini ya jinsi ya kupanua barabara katika eneo hilo ili kujenga vibanda hivyo vya wafanyabiashara.
RAS Morogoro hapa anapata maelezo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa eneo la Dumila
Akiwa katika eneo hilo la Dumila Mhandisi Emmanuele Kalobelo amesema agizo la rais limeanza kutekelezwa kuanzia leo, na Agosti kumi mwaka huu vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kazi hiyo vitawasili eneo la tukio na kuanza kazi.
Pamoja na kutoa ufafanuzi huo Katibu Tawala huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya kazi hiyo na kuanza ujenzi wake haraka badala ya kusubiria fedha zilizoahidiwa na Mhe Rais.
RAS Kalobelo akiongea na wafanyabiashara wa eneo la Feli Dumila - Morogoro
Mhandisi Kalobelo amewaagiza wataalamu Wanaochora michoro ya vibanda vitakavyojengwa eneo hilo kuhakikisha vibanda hivyo vinakuwa rafiki kwa makundi yote wakiwemo mama nitilie na baba nitilie pamoja na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ili makundi yote yaliyokuwa yanafanya biashara eneo hilo kutoathiriwa na mpango huo mpya.
Aidha, Mhandisi Kalobelo ametoa wito kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa pamoja na Wafanyabiashara wa eneo la Dumila, kutoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi wa vibanda hivyo na kuhakikisha msaada huo unawanufaisha wafanyabiashara halisi waliokuwa wanafanya biashara eneo hilo badala ya kuingiza watu wasiohusika au hawakuwepo hapo awali.
Bidhaa nyingine ambazo zinapatikana kwa wingi eneo la Feli Dumila Mkoani Morogoro
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale pamoja na kumshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa msaada wa shilingi 100Mil. za kuwajengea wafanyabiashara maeneo bora ya kufanyia biashara zao, amesema kazi aliyoiagiza Rais wameanza kuitekeleza kwa kuwatambua wafanyabiashara wa eneo la Feli - Dumila na kwamba watafanya kazi hiyo kwa umakini na haraka ili wananchi wanaohusika waweze kunufaika na msaada uliotolewa na Rais mapema.
Haya ndio mazingira ya Barabara ya Dodoma - Morogoro eneo la Dumila
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Nkolante Ntije, amesema agizo la Mhe. Rais pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara, lililenga pia usalama wa wafanyabiashara wa eneo hilo, hivyo wamependekeza vibanda vitakavyojengwa katika eneo hilo vijengwe upande mmoja wa kushoto wa barabara ukitokea Dodoma kwenda Morogoro ili kupunguza watu kukatisha mara kwa mara barabara hali inayoweza kusababisha ajali.
Baadhi ya Wataalamu na viongozi waliokuwepo eneo la Feli wakielekezana namna ya kazi ya ujenzi wa vibanda itakavyofanyika
Aidha, ameuomba uongozi wa Wilaya ya Kilosa ambao wana dhamana ya kutoa wataalamu wa kuchora michoro ya vibanda vitakavyojengwa eneo hilo, kuwapatia michoro hiyo mapema ili nao waanze kazi ya hiyo kwa haraka.
Mhandisi Kalobelo akiongea na vyombo vya Habari (havipo) mara baada ya kumaliza kutembelea maeneo yaliyoainishwa kujengwa vibanda.
Kwa niaba ya wananchi wa eneo la Feli Mwenyekiti wa kijiji cha Magole Hamad Athman Seleman ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati wakati wote wa ujenzi wa Vibanda hivyo na kwamba atasimamia ipasavyo mali zote zitakazoletwa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi, kwa kuwa mradi huo umeletwa kwa ajili yao na ni mali yao.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.