Balozi Seif ataka maandalizi kwa wanafunzi watakaosomea kilimo
Na: Andrew Chimesela, Morogoro
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd ameshauri kuwepo maandalizi ya wanafunzi kusoma masomo yanayohusu kilimo tangu wakiwa katika ngazi ya msingi badala ya wanafunzi wenye nia hiyo kukutana na masomo hayo wakati wakijiunga na Chuo Kikuu.
Balozi Idd ametoa ushauri huo Agosti 7 mwaka huu mara tu baada ya kutembelea vipando na mabanda ya Maadhimisho ya wakulima, wafugaji na wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika uwanja wa Mwl. Julius Nyerere eneo la Nanenane Mkoani Morogoro.
Akiwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo Balozi Seif alitembelea mabanda na vipando vya Halmashauri, Miji, Majiji na Taasisi mbalimbali za Serikali na za mashirika binafsi ambapo pia alitembelea banda la SUA na banda la wahitimu wa kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine - SUA ambao wamejiajiri baada ya kuhitimu masomo yao jambo ambalo lilimfurahisha Balozi Seif.
Hata hivyo Balozi Seif amesema ni vema wanafunzi wenye malengo ya kwenda kusomea Sekta ya Kilimo katika ngazi za juu wakaanza kuandaliwa mapema kupatiwa masomo yanayohusu Kilimo tangu wakiwa katika Elimu ya Msingi ili wajue vema nini maana ya kilimo kabla hata hawajajiunga na vyuo vikuu kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi katika Sekta ya Kilimo.
“Mwanafunzi wa Sokoinne ili kumpatia mwanzo mzuri wa kukijua hasa kilimo ni vema tukawaanzia tangu madarasa ya chini, walau kuanzia Primary, sehemu ya silabasi inakuwa Kilimo” alisema Balozi Seif.
Maadhimisho hayo ya 25 ya wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro yenye kaulimbiu “Wekeza katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa maendeleo ya Viwanda” yanatarajiwa kufikia kilele chake Agosti 8 mwaka huu ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri wa Mifugo Mhe. Luhaga Joelson Mpina.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.