SERIKALI YASEMA MABARAZA YA WAFANYAKAZI NI KIUNGO MUHIM
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Serikali imesema itaendelea kujali na kuzingaztia utaratibu uliopo wa kuwa na Mabaraza ya Wafanyakazi kwa kila Taasisi kwa kuwa mabaraza hayo ni kiunganishi muhim kati ya Menejimenti na Wafanyakazi ndani ya Taasisi za Serikali.
Hayo yamesemwa Julai 20 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare kwa niaba ya Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, alipokuwa akifungua kikao cha kwanza cha Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kilichofanyika katika Ukumbi wa TAFORI Mkoani hapa.
Amesema lengo la Serikali katika Taasisi zake ni kutaka kuleta mafanikio katika Nyanja zote zinazofanywa na wafanyakazi wake hivyo ili kufikia mafanikio chanya ni lazima kuwa na mahusiano mazuri baina ya waajiri na waajiriwa pamoja na kuwashirikisha Wafanyakazi mambo muhimu yanayofanywa na Taasisi husika.
“mathumuni ya kuwashirikisha watumishi ni kutaka kujadili na kuishauri serikali kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya ajira mahali pa kazi kwa lengo la kuleta tija” alisema Loata Sanare.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akifungua kikao cha kwanza cha Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, bila ushirikiano baina ya Mwajiri na Mtumishi ni vigumu Taasisi kutimiza malengo yake, hivyo Serikali bado inaamini kuwa Mabaraza ni kiungo muhim katika kuleta mafanikio hayo huku akisema mabaraza hayo yapo kwa mujibu wa Sheria. Hata hivyo amewatahadharisha watumishi kuwa ni vyema kabla ya kudai maslahi yao, kupima kwanza kiwango cha utekelezaji wa wajibu wao kwa mwajiri.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Prof. Carolyne Nombo (kushoto) akimkaribisha Mgeni rasmi alipowasili katika viwanja vya Tafori
Loata Sanare amesema kupitia Mabaraza yaliyopo kwenye Taasisi, Waajiri wataweza kupokea maoni ya watumishi na kuweza kufikia maamuzi sahihi ya namna ya kuboresha mazingira ya kazi na watumishi kwa jumla.
Ameongeza kuwa wajibu wa Mabaraza hayo kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na kuzingatia maadili ya Utumishi ili kuleta tija kwa watumishi, Waajiri na Watanzania kwa jumla.
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TIA wakiwa wanaimba wimbo wa "Mshikamano" bila kushikana mikono kwa sababu ya ugonjwa wa COVID 19.
Katika hatua nyingine Loata Sanare kwa niaba ya Waziri Philip Mpango ameipongeza Taasisi ya TIA kwa mafanikio makubwa waliyofikia katika kutoa Elimu yenye ubora ambayo imechangia kupata wataalamu wanaochangia katika Ujenzi wa Taifa la Tanzania.
Mwisho, amewataka Wakurugenzi, Mameneja wa Kampasi, Wakuu wa Vitengo na Idara kusimamia suala la maadili katika sehemu zao za kazi wakikumbuka kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuondoa vitendo vyote vya rushwa mahali pa kazi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Prof. Carolyne Nombo akimkaribisha Mgeni rasmi kufungua kikao hicho amesema majukumu makuu ya TIA ni kutoa mafunzo, ushauri wa kitaalam na kufanya tafiti timizi kwenye Nyanja za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi na maeneo mengine ya Biashara.
Prof. Nombo akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua kikao cha wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa TIA
Prof. Nombo amesema, utafiti unaofanywa na TIA kwenye baadhi ya Halmashauri hapa nchini, una mchango katika ukusanyaji wa mapato kwa kuwezesha Halmashauri hizo kuibua vyanzo vipya vya mapato na kubaini namna bora ya kudhibiti upotevu wa mapato kutokana na ukwepaji kodi na ushuru.
Aidha amesema, katika kikao hicho wajumbe wa Baraza hilo watapata fursa ya kupitia maazimio ya kikao cha Baraza lililopita, kuangalia mafanikio na kuweka vipaumbela kwa mwaka wa fedha 2020/2021 pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili na kupata majibu ya changamoto hizo.
Taasisi ya Uhasibu Tanzania ilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo, Ushauri na kufanya utafiti kwenye maeneo ya Uhasibu, Ununuzi na Ugavi na maeneo mengine ya kibiashara.
Hadi sasa Taasisi hiyo ina jumla ya wananfunzi 18,717 katika Kampasi zote sita hapa nchini ambazo ziko katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Singida, Mwanza, Kigoma na Mtwara.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.