Maafisa Ughani Morogoro Wapewa ushauri wa bure
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewataka Maafisa Ugani Mkoani humo kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine – SUA kutoa Elimu ya kilimo cha kisasa kinacholenga kuzalisha mazao mengi katika eneo dogo ili kuongeza tija kwa wakulima katika Halmashauri zao.
Mhandisi Kalobelo ametoa ushauri huo Julai 2 mwaka huu wakati wa maadhimisho ya siku ya wakulima ya Mradi wa RIPAT – SUA yaliyofanyika katika Kijiji cha Mlali Wilayani Mvomero ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya Kilimo walishiriki.
Mhandisi Kalobelo amesema moja ya sababu ukiachia mbali kupata mazao mengi katika eneo dogo bado teknolojia hiyo inasaidia kupata mazao yaliyobora tofauti na mazao yanayopatikana kwa kutumia kilimo cha kawaida, hivyo amesema ni vema Maafisa Ugani wa kila Halmashauri kuchukua Elimu hiyo inanyotolewa kupitia Mradi wa RIPAT – SUA na kwenda kuisambaza kwa wakulima katika Halmashauri zao.
Hata hivyo Mhandisi Kalobelo amesema wakati umefika sasa kwa kila mmoja hususani wakulima kuanza kukitumia ipasavyo Chuo Kikuu cha SUA ili kupewa mbinu za namna ya kuongeza tija zaidi katika mavuno.
“Nadhani ni wakati sasa kwa kila mmoja wetu, kuona umuhimu wa kuwatumia wataalamu wetu wa kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine kuweza kuona wanatuongezea tija namna gani katika uzalishaji wetu katika mazao mbalimbali” alisema Mhandisi Kalobelo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akiongea na wanakikundi cha TUKALEGOYA (hawapo pichani) alipotembelea shamba darasa la kikundi hicho
Akiongea na vikundi mbalimbali vya wakulima, Katibu Tawala huyo amewataka wakulima ambao wako kwenye mradi wa RIPAT – SUA kutumia teknolojia ya kilimo waliyoipata kupitia miradi mbalimbali inayofadhiriwa kupitia Chuao Kikuu cha SUA na sehemu nyingine kuwa ni nyenzo ya madhubuti kwao na jamii inayowazunguka badala ya teknolojia kuitelekeza mara mradi unapokoma.
“Tuna tatizo sisi watanzania wakati mwingine tunafundishwa kweli na tunajifunza kweli lakini tukisha toka hapa inakuwa kama maigizo sasa tusifanye Elimu tuliyoipata hapa iwe ya maigizo, twendeni tukaifanyie kazi. Aliongeza Kalobelo.
Mhandisi Kalobelo akipata maelezo ya utendaji kazi wa vikundi kutoka kwa Mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha SUA
Aidha, Katibu Tawala huyo amewatoa wasiwasi wakulima hao kuhusu changamoto ya kupata masoko ya mazao wanayozalisha ikiwemo viazi lishe na kuwataka kuendelea kuzalisha kwa wingi kwani Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ni sikivu iko tayari kulinda masoko ya mazao yao hata kwa kutunga sheria ndogo.
Mhandisi Kalobelo akiangalia aina ya maharagwe ambayo kilimo chake kina tija kwa wakulima kwa kuwa yana tabia ya kuzaa sana
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA Prof. Raphael Chibunda pamoja na kuwataka wanavikundi ambavyo viko kwenye mradi wa RIPAT – SUA kuacha mazoea ya kutelekeza teknolojia wanayopata bado amewaahdi wanakikundi cha TUKALEGOYA cha kijiji cha Mkuyuni Wilayani Mvomero pampu ya kumwagilia baada ya kuonekana ni changamoto kwao.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA Prof. Raphael Chibunda akitoa nasaha zake kwa wanakikundi cha mradi wa RIPAT - SUA. katikati ni Mratibu wa Mradi huo Dk. Emmanuel Malisa
Kwa upande wao Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mvomero Rehema Mhalule akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro waliowawakilisha Wakurugenzi katika hafla hiyo kwa kuwa mradi huo unatekelezwa ndani ya halmashauri hizo wameshukuru mradi huo kuongeza Elimu kwa wakulima wao na kwamba wataendeleo kutoa ushirikiano unaohitajika na kuendeleza mradi huo hata baada ya kufikia kikomo.
Wanakikundi cha Tukalegoya wakiwakaribisha wageni waliowatembelea kwenye shambadarasa lao
Mradi wa Jitihada shirikishi za kuleta mapinduzi ya kilimo Vijijini - RIPAT wenye Kaulimbiu “NJAA NA UMASKINI KUWA HISTORIA, INAWEZEKANA” unafadhiriwa na nchi ya Denmark ambao ulianza mwaka 2018 ukikusudia kusaidia jamii kukabiliana na njaa na umaskini.
Hadi sasa Mradi umekwishawafikia wakulima 650 kati ya 720 waliolengwa sawa na 90% kupitia vikundi mbalimbali vya wakulima ambavyo hadi sasa vimefikia 22, wanachama halisi ni 352 ambao wana hisa zenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 48.
Hili ni moja ya shamba la migomba la wanakikundi cha mradi wa RIPAT - SUA
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.