Waziri Mkuu kutuma timu kuchunguza sakata la DC, DED Malinyi
Na. Andrew Chimesela – Mahenge, Morogoro
Kufuatia kuwepo kwa mgogoro wa muda mrefu mkubwa kati ya mkurugenzi wa halmshauri ya wilaya ya Malinyi Musa Mnyeti na mkuu wa wilaya hiyo Majura Kasika waziri mkuu Kassim Majaliwa ameagiza mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali CAG, Wakala wa Majengo Tanzania TBA na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora kufika wilayani humo ili kuchunguza kwa kina kiini cha mgogoro huo.
Waziri Mkuu amesema hayo leo Septemba 16 wakati akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Toboa wilayani Malinyi, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
Waziri Mkuu amefikia hatua hiyo ili kufika katika Wilaya hiyo ili kuchunguza matumizi ya Mapato ya ndani yanayokusanywa katika Halmashauri ya Wolaya ya Malinyi, kukagua majengo yote ya miradi kama yanaendana na thamani ya fedha zilizotumika na kuchunguza chanzo cha maelewano hafifu baina ya Viongozi hao
‘’ Rais anateua viongozi wazuri , waadilifu, wasio wala rushwa, lakini nyie DC na Mkurugenzi wake mmekuja hapa badala ya kufanya kazi mnagombana, nasikia hamuivi chombo kimoja’’ alisema Waziri Mkuu.
Alisema kinachoshangaza viongozi hao wanafikia hatua ya kugombania miradi inayopelekwa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na hivyo kusababisha kushindwa kutekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu.
Hivyo, ameamua kumpeleka Wilayani humo CAG, Katibu Mkuu wa utumishi pamoja na wakala wa udhibiti wa majengo TBA ili kuchunguza na kutoa ripoti pamoja na kuishauri serikali nini kifanyike katika kuchukua hatua.
Amesema ni aibu sana kwa viongozi wa Serikali kuwa na mgogoro baina yenu hadi kufikia hatua ya kuwagawa watumishi, pamoja na wananchi katika kufanya shughuli zao ‘’ Mnakuja hapa hamfanyi kazi, mnagombana hicho mnachokitafuta ole wenu” ameonya.
Awali mbunge wa jimbo hilo Malinyi Dk. Mponda alimwambia Waziri Mkuu kuwa viongozi hao wamekuwa wakirumbana na kugombana waziwazi hali inayosababisha kuzorotesha maendeleo ya wilaya hiyo.
Waziri Mkuu akiwa wilyani Malinyi aliweka jiwe la msingi jengo la Ofisi za Halmashauri ya wilaya hiyo lenye thamani ya shilingi bilioni 3.9 linalojengwa na shirika la nyumba la Taifa NHC na kuwataka vijana wanaopata ajira katika mradi huo kutoharibu miundombinu yake wala kuiba vifaa vya ujenzi wa mradi huo ili waaminiwe .
Mwisho
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.