J.K. KUNOGESHA MAONESHO MOROGORO
Na . Andrew Chimesela – Morogoro
Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete anatazamiwa kuwa kivutio kwa wadau wa Maonesho ya Wakulima na wafugaji Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl. J. K. Nyerere Mjini Morogoro.
Maonesho hayo ali maarufu kama Nanenane ambayo yameingia leo ni ya nnetangu kuanza yanategemewa kunoga zaidi kutokana na ujio wa Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye kesho Agosti 5 anatarajiwa kutembelea mabanda ya maonesho ya Nanenane ya Kanda ya Mashariki Mjini Morogoro.
Baada ya Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo Bw. Ernest Mkongo kutoa taarifa ya ujio wa Kiongozi huyo wa Kitaifa mstaafu, mwandishi wa habari hii alipita kwa baadhi ya wananchi kupata maoni yao kuhusu ujio wa kiongozi huyo ambapo wengi walionekana kuhamsika kwenda katika viwanja vya Nanenane vya Mjini Morogoro kwa lengo la kumuona kiongozi huyo.
“Mimi sijaenda kwenye maonesho ya mwaka huu tangu yaanze lakini kesho nitakwenda ili pamoja na shughhuli zangu nyingine lakini pia nikamuone Ndugu Kikwete kwani tangu astaafu sijawahi kumuona” alisema Evancy Evarist mkazi wa Morogoro.
Aidha, Evanncy alisema Mhe. Jakaya Kikwete alikuwa kiongozi wa nchi ambaye alikuwa anategemewa na Watanzania wote pamoja na kuwa amestaafu lakini amesema hategemei kama kesho Kikwete akipewa nafasi anaweza kuongea ‘wrong statement’ (sentensi zisizo na maana) hivyo anataka kwenda kusikia anachoongea kwa sasa baada ya kustaafu kwake huku akisema anajua atakayoongea yatakuwa ya kuelimisha.
Maonesho hayo ya 25 ya Wakulima na Wafugaji Kanda ya Mashariki yanayojumuisha Mikoa ya Pwani, Tanga, Dar es Salaa na Morogoro yamefunguliwa Rasmi leo na Mhe. Charles Mwijage (MB) na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Akifungua Maonesho hayo Waziri Mwijage amesifu maonesho ya Mwaka huu ya Kanda ya Mashariki kuwa ni maonesho ya Kimataifa, na amesema kinachohitajika sasa ni kupeleka kwa wananchi teknolojia hiyo inayooneshwa kwenye maonesho hayo.
Sambamba na hilo, amewataka wadau wa maonesho hayo kufanya kilimo, Ufugaji na uvuvi kuwa sekta wezeshi kwa ajili ya kukuza Sekta ya viwanda kwa kuwa sekta ya viwanda ni soko la bidhaa zinazotokana na Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe akimkaribisha mgeni rasmi kufungua maonesho hayo, amesema kuna maendeleo makubwa ya ukusanyaji wa mapato ya Nanenane Kanda ya Mashariki wakati huu ambapo Sekretarieti za Mikoa zinaendesha na kusimamia maonesho hayo ya Nanenane.
Dkt. Kebwe amesema tangu mwaka jana Sekretarieti za Mikoa zilipokabidhiwa kuendesha maonesho hayo kwa Kanda ya Mashariki kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato wakati wa maonesho ambapo mwaka 2017 takribani shilingi Mil. 200 zilikusanywa wakati mwaka 2016 ambapo maonesho hayo yalikuwa yanaendeshwa na TASO zilikusanywa shilingi million 70 tu.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.