Dkt. kebwe apiga stop uongozi kiwanda cha magunia – morogoro
Na Andrew Chimesela - Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ameutaka uongozi wa Kiwanda cha kutengeneza magunia kilichopo Kihonda Mjini Morogoro kusimamisha mara moja zoezi la kutaka kupunguza wafanyakazi wa kiwanda hicho kwa kuwa zoezi hilo halijafahamika vizuri kwa wafanyakazi.
Mkuu wa Mkoa ametoa amri hiyo jana Juni 17 alipofika katika Kiwandani hapo na kufanikiwa kuongea na uongozi wa Kiwanda pamoja na baadhi ya wafanyakazi ambao walikuwa bado hawajaondoka kurudi majumbani kwao huku wakionekana kuwa na wasiwasi na paniki baada ya kusoma matangazo ya kuwepo kwa zoezi hilo la kupunguza wafanyakazi.
Dkt. Kebwe amesema ameamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu amepokea simu nyingi pamoja na ujumbe mfupi (sms) kutoka kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho wakilalamikia zoezi hilo kuletwa ghafla na kutojulikana vema maudhui yake.
Dkt. Kebwe amesema kiwanda hicho ndiyo kiwanda pekee katika nchi za Maziwa Makuu hivyo wanakiangalia kwa jicho la pekee na kwa uzito wa hali ya juu kwa sababu hiyo Uongozi wa Mkoa hauwezi kukubali kirahisi mabadiliko ya ghafla na bila uongozi kujua vizuri na hivyo kuamua kusimamisha zoezi hilo.
“Kwa hiyo waheshimiwa Menejimenti ya kiwanda zoezi hili lisimame kwa sababu halijaeleweka vizuri kwa watumishi na hata sisi ofisini hatulifahamu vizuri”
Akiongea kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Kiwandani hapo Bi. Marietha Kazimoto amesema baada ya kusikia taarifa hizo walikwenda kwa uongozi wa kiwanda kuuliza kama Uongozi ngazi ya Mkoa unajua mabadiliko hayo na kujibiwa kuwa hakuna haja ya uongozi huo kujua mabadiliko hayo.
Aidha, Bi. Magreth amesema sababu iliyopelekea wafanyakazi wengi kuwa na wasiwasi ni uharaka wa kufanyika zoezi lenyewe na kwamba baada ya zoezi, wafanyakazi watakaopunguzwa wanaweza kuingia mkataba na kufanyakazi kwa mwekezaji mwingine atakayeendesha kiwanda hicho lakini watatakiwa wawe na vitambulisho vya NIDA jambo ambalo limewatisha wafanyakazi wengi.
Kwa upande wao wafanyakazi wakiwemo Bw. Richa Stephano, Marcus Mathias na Queen Jackson wamemshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuingilia kati zoezi hilo na kwamba wanakubaliana na agizo alilotoa la kusimamisha zoezi hilo hadi pale litakapowekewa utaratibu unaotakiwa ambao hautaeta madhara makubwa kwa pande hizo mbili.
Kutokana na sakata hilo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ameunda Kamati ya watu Nane (8) ili kuchunguza kwa kina sakata hilo la Uongozi wa Kiwanda kutaka kupunguza wafanyakazi wa kiwanda hicho bila kutoa taarifa za uhakika kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho. Kamati hiyo ya watu nane inatarajia kutoa taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa hapo Juni 24, 2019.
Mwisho
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.