DKT. KEBWE AUNDA TUME KUCHUNGUZA SHILINGI MIL.76
Na Andrew Chimesela –Ifakara Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ameahidi kuuanda tume ya kuchunguza upotevu wa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi 76 Mil. ambazo inasemekana hazijulikani matumizi yake baada ya kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi cha Kibaoni katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero.
Dkt. Kebwe ametoa kauli hiyo Julai Mosi mwaka huu muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ufunguzi wa ujenzi wa Kituo kipya cha mabasi cha kibaoni kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara katika Wilayani Kilombero kilometa tano kutoka kilipo sasa kituo cha mabasi cha zamani cha Mji wa Ifakara.
Amesema, kuna fedha kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 76 ambazo miaka ya nyuma inaelezwa zilitumika katika kuendeleza eneo hilo ambalo linatarajiwa kujengwa kituo hicho cha mabasi ingawa matumizi yake hayako wazi, na kwa sababu hizo ni fedha za Serikali haiwezekani kulifumbia macho na kuahidi kuunda tume ili kujua ukweli wake na matumizi yaha hizo.
“Lakini kwa sababu ni hela ya Serikali hatuwezi kufumbia macho…., nitaunda kamati ya kufanya Audit, wapekuwe waone hele hiyo imetumika vipi na aliyeitumia awe amestaafu au awe amehama ajue hela hiyo ataitapika” alisema Dkt. Kebwe.
Aidha, Dkt. Kebwe ameagiza magari yote ya abiria yanayofanya biashara katika mji wa Ifakara kuanzia Julai 2, mwaka huu yaanze kutumia kituo cha mabasi cha Kibaoni ili kuongeza mapato ya Mji wa Ifakara na amepiga marufuku standi bubu na watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pamoja na maagizo hayo Kebwe ameutaka uongozi wa Mji wa Ifakara kutowasumbua wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga na mama nitilie, badala yake uongozi uwasajili ili watammbulike na kuachwa wafanye biashara zao katika soko hilo wakiwa huru. Aidha, ameupongeza uongozi huo kwa kutenga vyumba nane kwa ajili ya watu wenye mahitaji Maalum wakiwemo wazee ili kuendesha shughuli zao kwa lengo la kujiongezea kipato kupitia vyumba hivyo. Dkt Kebwe ameuagiza uongozi kutoa yvumba hivyo bure kwa kundi hilo.
Aidha, Dkt. Kebwe amesema ameunda kamati ya kufuatilia sakata la kugawana mali baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na Halmashauri ya Mji wa Ifakara. Taarifa ya Kamati hiyo aliyoiunda imemaliza kazi yake na italetwa na kusomwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro mbele ya viongozi wa Halmashauri zote mbili na hakutakuwa na mjadala katika maamuzi yaliyomo kwenye taarifa hiyo kwa kuwa taarifa imefuata mwongozo uliotolewa na Serikali unavyoelekeza namna nzuri ya kugawana mali hizo.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo pamoja na kukubaliana na ujenzi wa kituo cha mabasi cha Kibaoni, ameutaka Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuendelea kuweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi cha kisasa na cha kudumu kwa kuwa kituo cha Kibaoni baada ya kukamilika kwa barabara ya Kidatu - Ifakara hakitafaa tena kwa kuwa kutakuwa na watu na magari mengi kuliko ilivyo sasa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Mhe. Mashaka Mbilinyi amesema pamoja na kuwa mradi wa Kituo cha mabasi cha Kibaoni utaiingizia mapato Halmashauri yao bado alimemwomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kufuatilia mradi huo kwa karibu zaidi hususan matumizi ya shilingi Mil. 76.2 zilivyotumika siku za nyuma, huku Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Francis Ndulane akieleza lengo la mradi huo kuwa ni kupunguza msongamano wa magari katikati ya Mji wa Ifakara na kuzuia standi zisizo rasmi katikati ya Mji huo.
Mradi huo wa Kituo cha Mabasi Kibaoni ni mradi uliopokelewa na Halmashauri ya Mji wa Ifakara kutoka kwa Halmashauri mama ya Wilaya ya Kilombero, na eneo nzima lina ukubwa wa mita za mraba 8,550.
Haki Miliki © 2018 Mkoa wa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa