Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amerudia agizo lake alilolitoa Novemba Mosi mwaka huu la kuwataka wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu katika Msitu wa Hifadhi wa Namwai Wilayani Kilombero kuacha kufanya shughuli hizo na wale wanaofanya makazi katika msitu huo kuondoka mara moja.
Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki hii wakati wa ziara yake ya siku tatu ya kukagua shughuli za maendeleo na kusikiliza kero za wananchi hivyo kufanya Mkutano na wananchi wa Kijiji cha Kisegese Tarafa ya Namawala Wilayani Kilombero ambao wengi wao wanafanya shughuli za kibinadamu ndani ya msitu huo wa Hifadhi.
Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi wote wanaouzunguka Msitu huo wa Hifadhi kikiwemo Kijiji cha Kisegese kuheshimu mipaka iliyowekwa kuzunguka Msitu na yeyote atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua za sheria.
“lakini hawa ambao wamejipatia maeneo makubwa tena kwenye hifadhi, waache kufanya kazi hiyo tangu tarehe moja ambayo nilitoa maelezo wale ambao watang‘ang’ania kukaa huko watatolewa kisheria” alisema Dkt. Kebwe.
Aidha, Dkt. Kebwe amesema atawachukulia hatua za kisheria viongozi wote wa vijiji, hususan wa Kijiji cha Mofu na kijiji mama cha Namawala ambao wametajwa kuhusika kuuza maeneo makubwa ya Msitu wa Hifadhi wa Namwai huku wakijua kuwa huo ni Msitu wa Hifadhi hivyo kuwachonganisha wananchi na Serikali.
Wananchi kwa upande wao akiwemo Ester Simwanza wa Kijiji cha Ihenga moja ya vijiji vinavyouzunguka Msitu wa Hifadhi wa Namwai wameulaumu Uongozi wa Kijiji cha Mofu kwa madai ya kuwauzia wananchi wa kijiji hicho maeneo ya msitu huku wakijua ni Kosa.
Wananchi wengine walifika mbali zaidi na kukataa kuufahamu msitu wa Namwai kuwa sio hifadhi na kwamba eneo hilo wao wameliingiza kwenye matumizi bora ya ardhi na kutaka waachwe waishi humo kulingana na mpango walio nao.
Hata hivyo Afisa Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Bw. Joseph Mgana alikataa kuwepo kwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika Msitu huo na kwamba kama wana vielelezo vyenye Baraka kutoka Uongozi wa Halmashauri na Baraza la Madiwani kuhusu mpango huo waviwasilishe kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Nae Kaimu Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Bw. Magai Chomba alitaja shughuli zinazoendelea kufanyika ndani ya Msitu wa Hifadhi wa Namwai kuwa ni pamoja na Makazi, uwindaji haramu wa wanyama pori, uchomaji Mkaa, upasuaji holela wa mbao, kilimo , ufugaji ndani ya msitu na ukataji holela wa miti.
Msitu wa Hifadhi wa Namwai ni msitu pekee wa mapito ya wanyama (corridor) kutoka milima ya Udzungwa na Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Kilombero kuelekea pori la Akiba la Selous.
Mwisho
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.