Na Andrew Chimesela – Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Stephen Kebwe ameiagiza Kampuni inayojenga Soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kufanya kazi ya ujenzi huo usiku na mchana ili kufidia muda ambao wataweza kuupoteza wakati wa mvua za masika zitakapoanza kwa lengo la ukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo Januari 2 mwaka huu alipofanya ziara katika soko hilo akiambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ili kujiridhisha maendeleo ya ujenzi huo na kubaini kama kuna changamoto au mapungufu yoyote.
Katika kujiridhisha huko alibaini kuwa ujenzi huo uko nyuma ya ratiba ya kukamilika kwake kwa wiki tano, ndipo alipofikia hatua ya kuagiza ujenzi huo kufanyika usiku na mchana. “kwa hiyo nimewaelekeza wajenge usiku na mchana ili hata kama ikitokea bahati mbaya mvua zitakuja kwa wingi wawe wamekwisha okoa sehemu ya muda” alisema Dkt. Kebwe.
Naye Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro amewatoa hofu wafanyabiashara wa Manispaa hiyo kutekeleza makubaliano waliokubaliana awali kuwa wafanya biashara waliokuwa wanafanya biashara zao katika soko la awali watakuwa wa kwanza kupewa vizimba vya kufanyia biashara zao.
Kwa upande wake msimamizi wa Ujenzi wa soko hilo Mhandisi Antonio Mkinga alitaja changamoto za mradi ikiwa ni pamoja na eneo la mradi liko chini sana na kuwepo kwa mto Kikundi unaopita karibu na eneo hilo vinaweza kuathiri kwa kiasi mwenendo wa ujenzi huo jambo ambalo tayari Mkuu wa Mkoa amekwisha watahadharisha kuchukua hatua mapema katika kukabiliana na changamoto hizo.
Soko hilo kubwa na la kisasa ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania 17.6 Bil. ujenzi wake umefikia asilimia 15 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 19 mwaka huu.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.