Bakaa yamchefua RAS Morogoro, ataka hali hiyo kukomeshwa.
Na Andrew Chimesela, Morogoro.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewataka Maafisa Mipango na Wachumi Mkoani humo kutoendekeza mazoea ya kutotumia kwa wakati fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kusababisha fedha hizo kuvuka mwaka au kurudishwa hazina hivyo kutowatendea haki wananchi.
Mhandisi Kalobelo ametoa onyo hilo Oktoba 8 mwaka huu wakati akifungua Kikao cha Maafisa Mipango, Wachumi na Watakwimu wa Sekretarieti ya Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani humo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Veta katika Mji mdogo wa Mikumi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo (katikati) akisisitiza jambo wakati wa kufungua kikao cha Maafisa Mipango, Wachumi na Watakwimu, kilichofanyika VETA katika Mji mdogo wa Mikumi, Oktoba 8 mwaka huu. Picha na Andrew Chimesela
Amesema, kuna kasi isiyoridhisha kwa baadhi ya Maafisa Mipango na Wachumi ndani ya Mkoa huo katika utumiaji wa fedha za miradi ya Maendeleo hali inayoplekea kuwa na Bakaa kubwa wakati wa mwaka wa fedha unapofika.
“kumekuwa na kasi isiyoridhisha katika matumizi ya fedha za maendeleo hali inayopelekea kuwa na bakaa kubwa wakati wa mwaka wa fedha unapofikia mwisho, kwa mfano, hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2019/2020 kulikuwa na Bakaa iliyokuwa inafikia shilingi 9,430,444,666.00 kimkoa” alisema Kalobelo.
Amesema, kutotumia fedha za Serikali kwa wakati kama zilivyoelekezwa na Serikali ni kuwakosea haki wananchi na kupunguza thamani ya fedha zilizotolewa, kwa kuwa fedha hizo zikivuka mwaka hazitatekeleza mradi kama ilivyopangwa na kushusha thamani ya mradi wenyewe hivyo amewataka Maafisa hao kujipanga kukomesha changamoto hiyo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kalobelo, amewataka Maafisa hao kuwa na nidhamu katika kutekeleza maelekezo wanayopewa na viongozi wao hususan katika suala nzima la uwasilishaji wa taarifa mbalimbali, kwa kuwa baadhi yao wamekuwa na mazoea ya kuwasilisha taarifa hizo nje ya muda waliopewa na kusababisha adha kwa watumishi wengine na Serikali kwa jumla.
Wachumi kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro wakisikiliza kwa makini Hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa huo
Kuhusu uwasilishaji wa maombi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri zao kwa mwaka 2020/2021, Mhandisi Kalobelo ameagiza kila Halmashauri kuwasilisha taarifa hiyo kabla au ifikapo Oktoba 15 mwaka huu, na Afisa ambaye hatawasilisha taarifa hiyo tarehe iliyotajwa atachukuliwa hatua za kinidhamu.
“ikifika tarehe 15 mwezi huu wa kumi 2020, Afisa Mipango yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha hiyo taarifa mkoani kwangu nitachukua hatua kali za kinidhamu za uzembe, haiwezekani tuwe tunafanya kazi kwa ratiba zetu sisi wenyewe” alisisitiza Mhandisi Kalobelo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi, Idara ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Morogoro ANZAAMEN NDOSSA amesema, lengo la kikao hicho pamoja na mambo mengine kimelenga kukumbushana majukumu ya Maafisa mipango, Wachumi na Watakwimu, kutathmini utendaji wa kazi na kujifunza mbinu mpya za kuibua miradi yenye tija katika jamii.
Kuhusu changamoto ya bakaa, pamoja na kuiomba Serikali kupeleka fedha za Maendeleo mapema zaidi, Ndossa amesema Wizara ya Fedha imetoa mwongozo mpya wa namna ya kuomba fedha hizo, hivyo katika kikao hicho wataupitia mwongozo huo na kujipanga kuutekeleza mapema ili kuondoa changamoto ya kubakiza fedha zinazotolewa na Serikali unapofika mwisho wa mwaka wa fedha.
Nao washiriki wa kikao hicho akiwemo Jibril Mandari ambaye ni Mtakwimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero amekiri kupokea agizo la Katibu Tawala wa Mkoa la kutovusha fedha za miradi kutoka mwaka mmoja wa fedha hadi mwaka unaofuata kwa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kikazi baina ya Ofisi ya Mhandisi, Afisa Mipango na Ofisi ya Manunuzi kwa sababu Ofisi hizo ndizo zinazohusika kwa karibu kwenye masuala ya fedha za maendeleo.
Baadhi ya Washiriki wakiwa kwenye kikao hicho
Wakati huo huo Msifwaki Haule ambaye ni Afisa Mipango, ameelza sababu ya fedha kuvuka mwaka kuwa mara nyingi fedha zinazobaki ni zile zinazoletwa na Serikali mwishoni mwa mwaka yaani mwezi Juni pamoja na uwepo wa taratibu za nyingi za kimanunuzi, hata hivyo amekikiri kuyapokea na kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa na kiongozi wake.
Hii ndio Injini ya Mkoa wa Morogoro ambao wamejificha Mji mdogo wa Kitalii Mikumi, kwa lengo la kuweka mikakati ya namna ya kuupeleka mbele Mkoa wa Morogoro. Kutoka kushoto waliokaa ukimuacha mgeni rasmi, ni Mtakwimu Mkoa wa Morogoro, Anzaamen David Ndossa(Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu), Afisa Mipango wa Halmashauri ya Kilosa Bw. Kaunda, na Jacob Kayange ambaye ni Mchumi kutoka Sekretariet ya Mkoa wa Morogoro
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.