|
||||||||||||||||||||||
|
||||||||||||||||||||||||||||||||||
MIPAKA NA UKUBWA WA MKOA Mkoa wa Morogoro ni Mkoa wa pili kwa ukubwa hapa nchini ukitanguliwa na Mkoa wa Tabora. Mkoa una eneo la kilometa za mraba 73,039. Eneo hili ni sawa na asilimia 8.2 ya eneo lote la Tanzania Bara. Mkoa umepakana na Mikoa ya Pwani na Lindi upande wa Mashariki, Manyara na Tanga upande wa Kaskazini, Mikoa ya Dodoma na Iringa upande wa Magharibi na Mkoa wa Ruvuma upande wa Kusini. UMBILE LA ARDHI Umbile la ardhi ya Mkoa wa Morogoro linajumuisha milima ya Uluguru, Ukaguru, Nguru, Udzungwa na Mahenge. Mabonde na tambarare yamegawanywa na mito inayoanzia milimani. Baadhi ya mito hiyo ni Kilombero, Ruaha, Luwegu, Ruvu, Wami, Ngerengere, Mkindo na Mkondoa. Mito hiyo inafaa kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Kwa ujumla, ardhi ya Mkoa wa Morogoro ni nzuri na inafaa kwa kilimo cha mazao karibu yote yanayolimwa hapa nchini. UTAWALA Mkoa wa Morogoro kiutawala umegawanyika katika Wilaya tano ambazo ni Wilaya ya Morogoro, Mvomero, Kilosa, Kilombero na Ulanga. Kufuatana na Muundo wa Serikali za Mitaa Mkoa una Halmashauri za Wilaya tano na Halmashauri ya Manispaa moja ambazo ni Kilosa, Kilombero, Ulanga, Morogoro Vijijini, Mvomero na Manispaa ya Morogoro. Sambamba na kupeleka madaraka zaidi kwa wananchi Mkoa una mamlaka za Miji Midogo zinazofanya kazi za Gairo, Kilosa, Mikumi, Ifakara na Mvomero. Mkoa unayo majimbo ya Uchaguzi yenye Wabunge 10, Kata 141, Vijiji 543 na Mitaa 274 vitongoji 2,948 kama ilivyo katika jedwali HALI YA HEWA Hali ya hewa ni ya joto kati ya nyuzi joto 18 C katika sehemu za miinuko na nyuzi joto 30C katika sehemu za tambarare. Sehemu nyingi za Mkoa hupata mvua mara mbili kwa mwaka. Mvua za vuli hunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi katikati ya mwezi Januari, na mvua za masika huanza katikati ya mwezi Februari na kuishia mwezi Mei mwishoni. Kiwango cha mvua ni kati ya milimita 600 katika sehemu za tambarare na milimita 1,200 katika miinuko. Hata hivyo, zipo sehemu zilizo na ukame ambazo hupata mvua chini ya milimita 600 kwa mwaka. Sehemu hizo ni pamoja na Tarafa za Gairo na Mamboya katika Wilaya ya Kilosa na Tarafa ya Ngerengere katika Wilaya ya Morogoro.
|
|
||||||||||||||||||||||||
| Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, TEL: 026 - 2604237/2600973, FAX: 026 2601000 | ||