JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA      
   
     
     
 
 
HALMASHAURI YA WILAYA YA KILOSA
 
[ Nyumbani ]
 
[ MKUU WA WILAYA ] [ WABUNGE ] [HALMASHAURI YA KILOSA ] [ KATA & VIJIJI ]
 
                           
...............................................................................................................................................................................................................................................................................................................................................................................
         
 
Utangulizi
 

Wilaya ya Kilosa ilianzishwa rasmi mwaka 1926. Eneo la Wilaya ni kilometa za mraba 14,245 ikiwa ni sawa na asilimia 20.0 ya eneo la Mkoa wa Morogoro. Wilaya ipo Mashairiki mwa Tanzania kilometa 300 Magharibi mwa mji wa Dar es Salaam na inapatikana kati ya “Latitude” 5 ° 55' na 7 ° 53' Kusini mwa Ikweta na “Longitude” 36 ° 30' na 37 ° 3' Mashariki. Wilaya imepakana na Wilaya ya Kilombero na Mkoa wa Iringa kwa upande wa Kusini magharibi, Kaskazini imepakana na Mikoa ya Manyara na Tanga, Magharibi imepakana na Mkoa wa Dodoma na Mashariki Wilaya imepakana na Wilaya za Morogoro na Mvomero.

 
 
UMBILE LA ARDHI
 

Umbile la ardhi limegawanyika katika kanda kuu tatu, Kanda ya juu inayohusisha safu za milima ya Ukaguru na Nguru inayojitandaza kuanzia kaskazini kuelekea kusini ambayo ipo magharibi mwa Wilaya na ina mwinuko wa meta 2,200 kutoka usawa wa bahari. Chini ya milima hiyo ya kati na kusini mwa Wilaya ipo kanda ya uwanda wa tambarare na mabonde ya mito Wami, Mkata na Ruaha ambao uko kwenye mwinuko wa meta 400 kutoka usawa wa bahari. Kanda ya tatu iliyo kaskazini mwa Wilaya inayahusisha maeneo ya Gairo ambayo ipo katika mwinuko wa meta 1,100 kutoka usawa wa bahari.

 
 
 
IDADI YA WATU
 

Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, Wilaya ilikuwa na jumla ya watu 489,513 kati yao wanawake 245,312 na wanaume 244,201. Idadi hii ni sawa na asilimia 27.8 ya wakazi wote wa Mkoa wa Morogoro. Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 ilionyesha kuwa Wilaya ilikuwa na kaya 105,635 zenye wastani wa idadi ya watu 4.6 kwa kaya.

Aidha uwiano kijinsia ni wanaume 99 katika kila wanawake 100 kiwango ambacho kinaonyesha kuwa idadi ya wanawake ni kubwa kuliko wanaume.

 
Utawala
Halmashauri ina majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Kilosa, Gairo na Mikumi. Mhe. Greceford L. Mkunduge ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri na Bw. Ephraim Kalimalwendo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.
 
Sekta ya Kilimo
 

Wilaya inalo eneo la hekta 1,424,540. Eneo kubwa hutumika kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara kinachoendeshwa na wakulima wadogo wadogo vijijini pamoja na kilimo cha mashamba makubwa ya mkonge na miwa ambayo ni maarufu hapa Wilayani. Wilaya ina wafugaji na pia ina hifadhi ya misitu na mbuga ya wanyamapori.

 
Maeneo ya uzalishaji

Katika maeneo ya vijiji jumla ya hekta 4,612 zimegawiwa kwa wananchi 1,153 wenye uwezo wa kuyaendeleza ambapo kila mmoja alipata ekari 4

Upatikanaji wa pembejeo.

•  Mbegu bora
Mpango wa uzalishaji mbegu bora kwa kutumia wakulima wadogo katika vijiji 34 vya kata 28 umesaidia sana uzalishaji wa mazao yenye viwango bora kwa kutumia mbegu zilizothibitishwa na taasisi ya mbegu ya taifa (TOSCA).

•  Mbolea
Wilaya ya Kilosa ina hitaji jumla ya Tani 2,478 za mbalea. Kupitia mawakala 9 wenye maduka ya pembejeo jumla ya Tani 675.6 za mbolea ya ruzuku zimegawiwa kwa wakulima, Tani 10 ziligawiwa kwa wakulima wanaoshiriki kwenye mafunzo kupitia njia ya mashamba darasa. Mashamba ya mbegu ya Msimba tani 22.9, Kilangali tani Tani 7.5 kupitia ushirikishwaji wa wananchi wenye maduka ya pembejeo waliweza kutawanya na kuuza mbolea isiyo ya ruzuku jumla ya Tani 494.9 na kufanya mbolea yote iliyosambazwa msimu wa 2007/08 kuwa tani 1,210

 
Ushirika na Masoko
 

Wilaya ina jumla ya vyama vya Ushirika 68, Chama kikuu pamoja na vyama vya msingi vya mazao kwa wakati huu vinasinzia kutokana kutokuwa na mitaji ya kujiendesha ili kuviwezesha kukopesheka na kufanya biashara ya kununua, kusindika na kuuza mazao ya wakulima. Harakati zilizopo ni kushauri wanachama/wakulima hasa wa zao la pamba ili wajenge uwezo wa vyama vyao kwa njiia ya HISA kwa maana nzima ya kupata dhamana ya kupata mikopo toka vyombo vya fedha (kuweza kukopesheka).

•  Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo.

Vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo vilivyondikishwa ni 53 vyenye wanachama 11,505 wakiwemo wanawake 3,947 na wanaume 7,095. Katika vyama hivi kuna vikundi 271 na Taasisi 33. Kasi ya uandikishaji wa ushirika wa aina hii imekuwa kubwa kuanzia Julai 2006 hasa baada ya kutangazwa kwa dhana ya ujasiriamali/uwezeshaji. Kabla ya Julai 2006 SACCOS zilizokuwa zimeandikishwa zilikuwa 18, hivyo katika kipindi cha miaka miwili kuna ongezeko la SACCOS 35 sawa na asilimia 194.44. Katika utekelezaji wa nia ya kuwa na SACCOS katika kila Kata , Wilaya imefanikiwa kuandikisha SACCOS katika Kata 35 kati ya Kata 37 Kata mbili zilizobaki hatua ya uhamasishaji imekwishafanyika na wananchi wako katika hatua mbalimbali za ukamilishaji taratibu za kisheria ili uandikishaji ufanyike.

SACCOS 13 kulingana na mitaji yao zimeweza kupata mikopo nyenye thamani ya shilingi 959,600,000.00 toka katika taasisi za fedha

 

 
Elimu
 

Wilaya inalo Jukumu la kusimamia utolewaji wa Elimu ya Awali, msingi, sekondari kwa kuzingatia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES).Vilevile inatoa huduma ya uendeshaji wa Elimu ya Watu Wazima.

Malengo makuu katika utekelezaji wa Jukumu hili muhimu ni pamoja na haya yafuatayo:

•  Kuandikisha watoto wote wenye umri wa miaka mitano kuanza Elimu ya Awali – 2008.

•  Kuandikisha watoto wote 14,965 wenye umri wa miaka saba ili waanze darasa la kwanza, 2008 na walioandikishwa wanamaliza Elimu ya msingi.

•  Kuhakikisha kwamba vijana wote ambao hawakubahatika kuanza darasa lsa kwanza kwa wakati unaostahili wanaandikishwa katika madarasa ya MEMKWA.

•  Kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata nafasi ya kuanza.

•  Kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwa ni pamoja na kuzipa shule uwezo wa kifedha ili ziweze kujiendesha.

•  Kuhakikisha kwamba watu wazima wasiofika kusoma na kuandika wanapata fursa hiyo na pia wanajishughulisha na kazi za uzalishaji mali

 
Elimu ya Awali

Idadi ya shule za Awali zilizopo ni 149 zenye wanafunzi 8,193 wakiwemo wasichana 4,209 na wavulana 3,984.

Shule 146 ni za Serikali na zipo ndani ya shule za msingi na tatu nii za bianfsi. Shule za msingi zisizokuwa na shule za awali ni 65 ambazo maandalizi ya kuwa na shule hizo yatakamilika Desemba, 2009.

Hamasa imeendelea kutolewa kwa watu binafsi, Taasisi na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi kuanzisha shule za awali ili kuongeza huduma ya utolewaji wa elimu ya awali.

Elimu ya Msingi

Shule za msingi 220 zinatoa huduma ya Elimu ya msingi katika Wilaya hii. Kati ya shule hizo, 217 ni za Serikali na tatu (3) ni za binafsi na zinatumia lugha ya kiingereza katika kufundisha.

(iv) Uandikishaji wa darasa la kwanza.

Hali ya uandikishaji wa watoto wanaostahili kuanza darasa la kwanza imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Hii inatokana na uhamasishwaji wa kutosha wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu na kwa kiasi fulani ubora wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Idadi ya watoto walioandikishwa kuanza darasa la kwanza kwa kuzingatia umri wa miaka saba hadi kumi
 

Walimu wa Shule za Msingi

 

Mahitaji halisi ya walimu ni 2427. Waliopo ni 1874 na hivyo upungufu ni 553, sawa na asilimia 22.8. Kwa idadi hioyo ya wanafunzi uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi ni 1:58 wakati uwiano wa kitaifa ni 1:40 au 1:45.

 
Maji

Wilaya Kilosa imekuwa ikijishughulisha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini na mijini.

Kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 idadi ya watu wanaofadika na maji safi na salama imeongezeka kutoka watu 252,859 sawa na asilimia 52.0 mwaka 2005 hadi watu 275,106 sawa na asilimia 56.2 mwaka 2008 hali ambayo inaonyesha ongezeko la asilimia 4 kwa kipindi hicho. Aidha katika kipindi hiki vyanzo vikuu vinavyotumika kutoa huduma ni pamjo na visima vifupi, visima virefu, miradi ya maji ya bomba, uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia matenki, mabwawa (malambo) na maji ya mteremko (Gravity). Mchoro namba 4 hapa chini unaonyesha ongezeko vyanzo vinavyo toa huduma hii ya maji kwa Wilaya ya Kilosa katiya mwaka 2005 na 2008.

Pamoja na upatikanaji wa huduma hii ya maji, Wilaya inavyo vyombo vingine vinanyosimamia utoaji wa huduma hii.

Jumuia hizi zipo katika vijiji vya Msimba, Nguyami, Mkalama, Chanzuru, Twatwatwa, Meshugi, Mtumbatu, Mandela (Mabana, Mbigili na Mandela), Kitange II na Magole.

Changamoto

Changamoto iliyopo mbele yetu ni kuendelea kuhamasisha na kushirikisha jamii kuendelea kutunza vyanzo vyote vya Maji vilivyokwisha bainishwa Wilayani kwetu ili kutunza, kulinda na kuchangia huduma ili rasilimali hii muhimu iwe endelevu.

 

 
Mifugo

Utangulizi

Ufugaji ni moja ya shughuli ya kudumu katika Wilaya. Mifumo ya ufugaji inayoendeshwa Wilayani kilosa ni aina mitatu:-

•  Ufugaji huria ambao ndiyo mkubwa kwa kundi la ufugaji wa asili katika Tarafa za Magole, Kimamba na Masanze.

•  Mchanganyiko wa mifugo ya asili na kilimo cha mazao katika tarafa za Gairo, Nongwe na sehemu ya magharibi ya Tarafa za Magole, kidete na Mikumi.

•  Ufugaji wa ndani kwa ng'ombe na mbuzi wa kisasa wa maziwa na Nguruwe katika tarafa ya Kilosa Mjini, Kimamba, Ulaya, Mikumi, Magole,Gairo, Kidete na Masanze.

Usambazaji wa ng'ombe wa maziwa kwa wananchi umefanyika kupitia mradi wa HPT(Heifer International Tanzania) kwa udhamini wa mashirika ya dini ya KKKT na ACT kwa utaratibu wa kopa ng'ombe lipa ng'ombe ambapo jumla ya ng'ombe wa maziwa 339 wamegawiwa kwa vikundi 18 katika vijiji 18.Wilayani na pia jumla ya mbuzi wa maziwa 89 wametolewa kwa vikundi 2 katika vijiji 2 kwa utaratibu huo huo wa kopa mbuzi lipa mbuzi, utaratibu huu unaendelea kwa kugawa ndama majike na vitoto vya mbuzi vijike vinavyoendelea kuzaliwa kwa wananchi wanaohitaji.

ii) Kuboresha mifugo

Wilaya inao mpango wa muda mrefu w kuboresha mifugo ya asili kwa kutoa ya kisasa.

Shughuli ya uhamilishaji imeanza kufanyika ili kuongeza ubora wa ng'ombe wa maziwa ambapo jumla ya ng'ombe 40 mpaka sasa wamepandishwa na upandishaji unaendelea.

Mwaka wa fedha 2008/2009 Wilaya inakusudia kuanzisha mashamba darasa manne katika vijiji vya Twatwatwa, Mabwegere, Mbwade na Mfilisi ya unenepeshaji wa ng'ombe (yaani feed lot system) kwa lengo la kupata mifugo bora yenye kukidhi soko la ndani na nje kwa kuzalisha mazao ya nyama na ngozi za viwango vya juu.

Kwa mujibu wa sensa ya Wilaya iliyofanyika mwaka 2000/2001 na uboreshaji wa takwimu uliofanyika mwaka 2007 Wilaya ina zifuatazo za mifugo kama Jedwali namba 11 linavyosha hapa chini.
 
 
Viwanda, Biashara na Masoko

Wilaya ya Kilosa ina kiwanda kikubwa kimoja ambacho ni cha kutengeneza Sukari cha ILOVO, pia Wilaya ina viwanda vya kati vya katani

Kuna viwanda vya kutengeneza sukari gulu ambavyo ni.

•  Magole - Salal S Salehe

•  Mhenda - S.N.S.T.S – Silum

•  Mvumi - Mohsin M nalidi

•  Myombo - Said Khamis

•  Kisanga - N.S. Nahdi

Pia Wilaya ina viwanda vidogovidogo 313 vinavyohusisha viwanda vya uselemara, kukamua mafuta ya mbegu, mashine za kusaga, ushonaji na usokotaji.

Matumizi ya Vipimo.

Wilaya inasimamia Sheria ya vipimo namba 20 ya mwaka 1982 na marekebisho yake juu ya matumizi ya vipimo batili katika biashara kwa wakosaji wanaowaibia wananchi. Hii inahusu ufungaji wa magunia ya lumbesa, kikofia pamoa na utumiaji wa makopo, ndoo za plastic, sadro n.k katika biashara ni kunyume na sheria ya vipimio sura Na. 340 ya sheria ya Tanzania (co 340 R.E 2002) ambayo inawataka wafanyabiashara wote kutumia vipimo vinavyokubalika kisheria wakati wa kununua au kuuza bidhaa mbalimbali na wote wanaokiuka wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Ofisi ya vipimo imetoa ufafanuzi wa uzito wa juu kwa gunia kwa kilo 100.

 
 
 
 
 
 
AFYA

Wilaya Inakabiliwa na magonjwa makuu Malaria likiwa linaongoza. Pamoja na juhudi zilizochukuliwa na Wilaya kupambana na tatizo hili kama kusambaza hati punguzo kwa watoto chini miaka mitano na kwa mama wajawazito, SP kwa kinamama wajawazito na elimu ya afya katika kuboresha mazingira, bado ugonjwa wa malaria ni tatizo kubwa kwa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito.Hali halisi ya ugonjwa huo na mengine ni kama ilivyoainishwa katika jedwali namba hapa chini.

Magonjwa

Idadi

Asilimia

Malaria

26,668

48

Magonjwa njia ya hewa

11,983

21

Kichomi

4,765

8.6

Magonjwa ya kuharisha

3,798

6.8

Magonjwa ya ngozi

2,412

4.3

Magonjwa ya Macho

1,156

2.0

Magonjwa ya Masikio

692

1.2

Majeraha madogomadogo

540

0.9

Upungufu wa damu

351

0.6

Utapiamlo mkali

62

0.1

 

MMAM

Wilaya katika kutekeleza mpango wa MMAM, inatarajia kukarabati na kujenga vituo vya kutolea huduma za afya na upatikanaji wa vifaa/dawa/usafiri/mawasiliano kwa gharama ya shilingi 29,610,000,000.00 na watumishi

Mikakati ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM)

•  Kuongeza idadi ya wataalam wa afya katika zahanati na vituo vya afya vyote kwa kuajiri Wataalam wapya.

Katika kipindi cha mwaka mpya wa fedha halmashauri ya Wilaya inategemea kupata

kibali toka menejementi ya utumishi wa umma ya kuajiri jumla ya watumishi wa afya

wapya wa kada mbalimbali.

•  Kuwaendeleza watumishi mbalimbali walipo kazini

Pia jumla ya watumishi wa afya 32 wapo katika vyuo mbalimbali vya masomo vya kada ya afya katika mwaka huu wa fedha 2007/2008. Pia Wilaya imeandaa mpango wa mafunzo kwa watumishi hivyo jumla ya watumishi 126 wa kada mbalimbali wataendelezwa na kugharamiwa mafunzo yao katika vyuo mbalimbali kati ya mwaka 2007/2008 mpaka 2009/2010 hasa wale wa kada za chini kama wahudumu wa Afya wenye nia ya kujiendeleza na kada zinazotoweka kama Tabibu wasaidizi na MCHA. Baadhi ya watumishi watagharamiwa mafunzo yao wakiwa kazini (distance learning education) katika vyuo vya mbalimbali nchini.

 
 
Kampeni ya kitaifa VVU

 

Kampeni ya Kitaifa ya upimaji VVU kwa hiari

Wilaya ilifanya zoezi la upimaji wa VVU kwa hiari kuanzia mwezi Oktoba 2007 mpaka Juni 2008. Lengo lilikuwa ni kupima watu 60,021. Kutokana na wanchi kuhamasika tumeweza kuvuka lengo kufikia watu 60,382 sawa na 100.6% wakiwemo wanawr4rtake 31,469 na wanaume 28,914.

Kwa Wilaya yetu kiwango cha maambukizi kimefikia 4.0%, na maeneo yaliyoathirika zaidi ni Mikumi, Kidodi, Gairo, Dumila, Kimamba, Kilosa Mjini, Magomeni, Ulaya na Malolo. Maeneo haya yote ni maeneo yenye tabia za kimji na yenye mikusanyiko mikubwa ya watu. Aidha maeneo au kata ambazo hajawa na ushiriki mkubwa wa VVU/UKIMWI Chanjale, Nongwe, Chagngwe, Mandege, na Vidunda. Hali hii inatokana na kuwa maeneo haya yapo pembezoni na miji na haina mwingiano mkubwa wa jamii.

 
 
 
Barabara

Ili watu waweze kukutana nyenzo muhimu ni njia za mawasiliano kama vile; barabara, reli anga na maji. Wilaya ya Kilosa ina mtandao wa barabara zenye urafu wa km. 1,415 wa mgawanyo ufuatatao:

•  Barabara kuu km. 290,

•  Barabara ya Mkoa km. 209

•  Wilaya km. 446 na

•  Vijiji km. 470

Kati ya hizo km. 499 ni mtandao wa Kitaifa na Kimkoa na matengenezo yake yako chini chini ya Mkoa. Barabara hizi ni za kiwango cha lami na changarawe na hupitika kwa kipindi cha mwaka mzima. Km. 916 ni za Wilaya, kati ya hizo 724 ni za udongo na km. 192 ni za changarawe na matngenezo yake yanatokana na vyanzo vifuatavyo

•  Mfuko wa Barabara (Road Fund)

•  Mfuko wa Maendeleo wa Jamii (TASAF)

•  Mfuko wa Maendeleo wa Serikali za Mitaa (LGCDG)

•  Nguvu za wananchi

Barabara hizi ni za vijijini hupitika kwa urahisi kwa kipindi cha kiangazi na shida kwa kipindi cha mvua za masika, hivyo kufanya usafiri na usafirishaji kuwa mgumu hasa katika maeneo ya Mlunga, Uleling'ombe, Chagongwe, Leshata, Nongwe, Chanjale, Vidunda, Madududmizi, Tindiga na Chogolali. Mtandao mkubwa wa barabara zetu zinahitaji matengenezo makubwa. Kwa kuzingatia sera ya sekta ya hii Wilaya inalenga kuimarisha na kujenga miundo mbinu kwa kuzingatia mazingira na teknolojia muafaka ili kuimarisha njia za usafirishaji Mjini na vijijini. Wilaya imejiwekea mikakati ya kujenga na kukarabati barabara za Wilaya na vijiji kwa kushirkiana na wananchi, wahisani, na serikali kuu kupitia mfuko wa barabara.

Pamoja na barabara kuna njia ya reli ya kati ambayo hupita katikati ya Wilaya kutoka Magharibi hadi Mashiriki, ikiwa na vituo 6 ambavyo ni Mkata, Kimamba, Kilosa, Munisagara, Mzaganza na Kidete. Pia tuna kiwanja kidogo cha ndege kilichopo Magomeni Kilosa.

 
 
Hifadhi ya Mazingira

•  Wilaya ya Kilosa inayo mistu yenye ukubwa wa hekta 935,535 kama ifuatvyo:

•  Misitu ya kupandwa hekta 8,535

•  Misitu ya asili hekta 927,000

•  Licha ya kuwepo kwa hali hiyo, uharibifu wa mazingira kutokana na uchomaji wa mato, ukataji wa miti kwa ajili kilimo na uchomajia wa mkaa.

•  Shughuli nyingine inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira katika Wilaya ya kilosa ni Ufugaji holela na wingi wa mifugo ambayo imetoka nje ya Wilaya ya Kilosa. Wilaya imekuwa ikipokea isivyohalali kiasi kikubwa cha mifugo kutoka nje ya Wilaya. Maeneo ya misitu ya hifadhi ya maji kama Ukwiva, Palaulanga, Mamiwa ndiyo yaliyo athirika zaidi.

(ii) Kupambana na uharibifu wa mazingira

Kila mwaka Wilaya ya Kilosa huotesha na kupanda jumla ya miti 1,500,000 katika maeneo mbali mbali ya Jamii ikiwa ni wastani wa miti 10,000 kwa kila kijiji. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita yaani kuanzia mwaka 2005/06 – 2007/08 jumla ya miti 2,730,000 ilioteshwa, kusambazwa na kupandwa katika maeneo ya vijiji, Shule za msingi, taasisi mbali mbali na wananchi. Vile vile Wilaya imekuwa ikipanbana na uharibifu wa mazingira kwa kutumia sheria ndogo za Halmashauri.

Maendeleo ya Uvuvi

Uvuvi unaendeshwa na wavuvi wadogo wadogo katika mito na mabwawa. Ipo mito minne (4) na mabwawa ya asili 6, Mbuga za maji mengi - 2 na bwawa moja (1) la mdau.

Wilaya imefanikisha kutoa mbegu bora za samaki aina ya perege (Tilapia) ambayo ina uwezo wa kupata uzito wa gram 500-1000 kwa samaki mmoja. Ukuaji huu wa samaki umechangia katika kuwaongezea kipato na lishe bora kwa Wakazi wa maeneo jirani na mji wa Kilosa.

Tangu mwaka 1998 Wilaya ilianza kueneza elimu ya ufugaji wa Samaki katika vijiji

mbalimbali Wilayani na hadi sasa tayari mabwawa 230 yamesha Chimbwa na

wakulima hususani katika vijiji vya Lumbiji, Masenge, Mkobwe, Malolo, Vidunda na

Chagongwe. Maeneo haya yana mito ya kudumu na miundo mbinu ya mwagiliaji.

Wastani wa samaki tani 50 wenye thamani ya shilingi 75,000,000.00 huvuliwa kwa mwaka na aina kuu za samaki wanaovuliwa hii ni Kambale na Perege.

Ufugaji wa Nyuki

Wilaya ina utajiri mkubwa wa misitu kw ajili ya ufugaji wa nyuki, karibu asilimia 57 ya eneo a Ardhi limefunikwa na misitu yenye mtandao (network) nzuri yenye mito 11 mikubwa kama Mkondoa, Miyombo, Ruaha, Rudewa na Mkata, pamoja na mabwawa na vijito na hali ya hewa nzuri kwa ajili ya ufugaji nyuki. Maeneo yanayoelweka kwa ufugaji nyuki ni Tarafa za Gairo na Magole. Kwa sasa Wilaya ina jumla ya wafugaji 2,388 kati ya hao wnawake ni 236 na wanaume ni 2,152. ipo mizinga ya nyuki 19,764, kati ya hiyo 18,355 ni mizinga ya asili na 1,409 ni mizinga ya kisasa. Wilaya huzalisha Tani 317.6 za asali na tani 21.2 za nta kwa mwaka na hivi sasa uzalishaji ni asilimia 3.5 tu.

Changamoto zinzoikabili sekta ya Maliasili

Changamoto kubwa zinazotukabili ni pamoja na;

•  Ukosefu wa watumishi, hivi sasa Wilaya ina mtumishi mmoja tu wa Nyuki
•  Ukosefu wa mitambo ya kutengeneza mazao ya nyuki.
•  Ukosefu wa soko lenye uhakika.

Pamoja na changamoto hizo Wilaya inajitahidi kutatua baadhi ya matatizo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ambapo Wilaya imefanikiwa

•  Kutoa elimu bora ya ufugaji nyuki kwa vijiji 20, ikijumuisha watu binafsi na vikundi
•  Imeanza mchakato wa kuanzisha hifadhi za nyuki tatu katika vijiji vya Ilakala tarafa ya Ulaya, Ihombwe na Malolo tarafa ya Mikumi.
•  Kutoa msaada wa zana za kisasa za ufugaji nyuki ikiwa ni pamoja na mizinga na zana za kufanyia kazi kwa vijiji 12 katika Tarafa za Kimamba, Kilosa, Ulaya na Mikumi kwa kushirikiana na wadau wa mashirika ya WWF, Mfuko wa TASAF na CEPT pamoja programu ya PFM.

 
 

Ardhi

Wilaya imepima mipaka ya vijiji 109 pia ina mpango wa muda mrefu wa kutenga maeneo katika vya kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

•  Vijiji vilivyoandaliwa mpango wa matumzi bora ya Ardhi kipindi cha mwaka 2007/08 ni 12 ambavyo ambavyo ni pamoja na Twatwatwa, Mbwade, Msowero, Changarawe, Kivungi, Ruaha, Kitinga, Tundu, Iwemba, Lumango, Vidunda na Msowero Ruhembe.

•  Vijiji vilivyokuwa kwenye mpango wa kuandaliwa matumizi bora ya Ardhi kipindi cha mwaka 2007/08 ni Magubike, Berega, Kitange II, Meshugi, Kitaita, Kinyolisi, Ndogomi, Leshata, Malangali na Tindiga

Upimaji wa viwanja

•  Wilaya ya Kilosa imepima jumla ya viwanja 231

•  Hakuna vyeti vya Ardhi vilivyotolewa kwa kipindi cha mwaka 2005/06 – 2007/08 kwani bado hatuna masijala za kuweza kutunzia

•  Utoaji wa Hati Miliki 39 za Mashamba

•  Barua 17 za toleo za mashamba kwa kipindi cha 2005/06 – 2007/08 ziliandaliwa na kupelekwa Wizarani lakini Hati hazijatoka, zinasubiri idhini ya Kamishna wa Ardhi.

Utwaaji wa mashamba yasiyoendelezwa

•  Wilaya ina mashmba yasiyoendelezwa yana ukubwa wa hekta 8,301

 
 

Mawasiliano

Wilaya inawasiliana na sehemu zingine ndani na nje ya nchi kupitia radio, magazeti, simu za mkononi za mitandao ya VODACOM, CELTEL, TIGO, ZANTEL na TTCL, televisheni na tovuti. Wilaya ina kituo cha Radio (Radio Jamii Kilosa) na televisheni vinavyomilikiwa na Halmashauri. Matarajio ni kuwezesha radio na televisheni visikike Wilayani kote na nje ya Wilaya yetu kwani kwa sasa vinasikika kwa baadhi tu ya maeneo yaliyo karibu. Pia tuna vituo vya telecentre viwili vilivyoko kwenye chuo cha Vijana Ilonga na Kilosa mjini mahali ambapo vijana na wakazi wengine hufika na kujifunza matumizi ya kompyuta kwa gharama nafuu.

 

 

 

 

 

 
 
 
     
 
 
         
 
[ Nyumbani ]
Rudi juu
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, TEL: 026 - 2604237/2600973, FAX: 026 2601000